2016-12-08 14:25:00

Papa Francisko: Semeni ndiyo kwa Mungu na hapana kwa dhambi!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwenye Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka, ifikapo tarehe 8 amesema, Liturujia ya Neno la Mungu  katika maadhimisho haya inaonesha uhusiano wa kihistoria kati ya Mwenyezi Mungu ni binadamu; na kama mchakato unaompelekea mwanadamu kutambua kiini cha wema na ubaya!

Hapa mwanadamu anaoneshwa jinsi alivyoukana ukuu wa Mungu na kuamua kujitazama mwenyewe, kiasi hata cha kuvunjulia mbali muungano na Mwenyezi Mungu. Huu ukawa ni mwanzo kwa mwanadamu kuwa na woga na wasi wasi katika maisha yake; akaanza kujificha na kutoa shutuma kwa jirani yake, kielelezo cha dhambi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, hakupenda kumwacha mwanadamu kuogelea katika ubaya wa dhambi na mauti, katika hali ya utulivu na uvumilivu mkubwa akamwita Adamu na kumuulizia yuko wapi, ili aweze kurejesha tena uhusiano na binadamu kama ilivyokuwa hapo awali.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Injili ya Siku inamwonesha Bikira Maria aliyekubali mpango wa Mungu kuja kukaa kati ya watu wake, pale alipokubali kupokea ujumbe wa Fumbo la Umwilisho! Tangu wakati huo, Yesu akaanza hija ya maisha yake kuwaelekea binadamu. Bikira Maria akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu kwa muda wa miezi tisa! Akawa sawa na binadamu katika mambo yote, isipokuwa hakutenda dhambi! Bikira Maria aliteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu kwani hakuwa na doa la dhambi, alikuwa ni “Immakulata”, yaani Mkingiwa Dhambi ya Asili, alijaa neema na wala doa la dhambi halikuwa na nafasi katika maisha yake, alifunikwa na kilele cha uzuri.

Bikira Maria akamjibu Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe ulivyo nena”!. Hili ni jibu la ndio lisilokuwa na masharti hata kidogo kiasi cha kufungua njia ya uwepo wa Mungu kati ya waja wake, kinyume kabisa cha Adamu aliyeweka kizingiti katika mahusiano na Mwenyezi Mungu. Unyenyekevu wa Bikira Maria unageuza na kubwaga kiburi cha binadamu; ndiyo yenye uaminifu inaganga na kuponya ukosefu wa utii; majitoleo na sadaka vinashinda ubinafsi na dhambi.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, hata katika historia ya maisha ya kila mwamini kuna ndiyo inayomkubali Mungu na hapana inayomkataa Mungu. Wakati mwingine waamini ni hodari kwa kujifanya kwamba, hawatambui kile ambacho Mungu anataka kutoka kwao na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu. Ni wagumu kusema hapana lakini daima wanatafuta njia za kuhailisha maamuzi yao kwa kujisingizia kwamba, kesho watakuwa ni watu wema zaidi, watakuwa ni wachamungu kwa kusali zaidi; watatenda mema, lakini wanaendelea kufunga lango la wema na uzuri kwa kushindwa kusema ndiyo ya dhati inayotoka katika sakafu ya moyo wa mtu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kila ndiyo ya kweli na thabiti inakuwa ni mwanzo wa historia mpya! Kumbe, waamini wajifunze kusema ndiyo kwa Mwenyezi Mungu na hapana kwa dhambi inayowazeesha kutoka katika undani wa maisha yao. Kila ndiyo ya kweli kwa Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya historia ya wokovu kwa waamini wenyewe na kwa watu wengine. Katika safari ya kipindi cha Majilio, Mwenyezi Mungu anatamani kuwatembelea waja wake na anasubiri ndiyo yao kwa kusema “Ninakuamini” “Ninakutumainia” “Ninakupenda” na mapenzi yako yafanyike ndani mwangu. Kwa mfano na ukarimu wa Bikira Maria, kina mwamini leo hii amwambie Mwenyezi Mungu Ndiyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.