2016-12-08 09:07:00

Msindikizeni Dr. Magufuli kwa sala na dua njema katika utumishi wake!


Viongozi wanapaswa kusimama kidete ili kuhakisha kwamba, misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa vinalindwa na kudumishwa na wote. Ni wajibu wao kusimamia haki msingi za binadamu, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi pamoja na kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni sauti ya wanyonge na maskini ambao kutokana na vitendo vya rushwa na ufisadi, wanapokwa haki zao msingi. Ni wajibu wa viongozi wa Serikali kuwa mstari wa mbele ili kudumisha: nidhamu, miiko ya uongozi, kanuni maadili, uongozi bora na utawala wa sheria mambo msingi katika kukuza na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi!

Kutokana na changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza nchini Tanzania hasa wakati huu wa uongozi wa serikali ya awamu ya tano, Rais John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wenzake wanapaswa kusindikizwa kwa njia ya sala na dua njema, ili kweli waweze kutenda kwa hekima na busara, daima wakiweka ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote mbele yao. Wawe ni wachaji wa Mungu, kwa kuwa na hofu ya Mungu ambaye ndiye kiongozi mkuu wa watu wake!

Rais Magufuli katika uongozi wake ameendelea kujipambanua kuwa ni kiongozi anayesimamia ustawi na maendeleo ya wengi, hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu ambao kwa miaka mingi hawakupewa kipaumbele cha pekee na matokeo yake: rushwa na ufisadi vikatawala na kuivuruga Tanzania na hivyo kusababisha mipasuko ya kijamii kwa baadhi ya watu wachache kuwa na utajiri mkubwa wakati maelfu ya watanzania wakiendelea kudidimia katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato!

Hivi karibuni, Bwana Antony Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliwasihi watanzania kumkumbuka na kumwombea Rais Magufuli na viongozi wenzake wa awamu ya tano ili waendelee kurejesha nidhamu, maadili na kanuni za utumishi wa umma, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Watanzania na watu wote wenye mapenzi mema wawe mstari wa mbele kumuunga mkono Rais Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; dhidi ya utendaji wa kazi kwa mazoea, ili Tanzania iweze kucharuka si tu kwa maendeleo ya viwanda, bali katika utu na heshima kama binadamu mwenye haki na nyajibu zake.

Viongozi wa Serikali na watumishi wa umma watambue kwamba, wamepewa dhamana ya kuwahudumia watanzania katika misingi ya haki, ukweli na uwazi. Lakini, ikumbukwe kwamba, maendeleo na ustawi wa watanzania vitachochewa kwa kiasi kikubwa ikiwa kama misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano vitatawala na kudumishwa katika akili na nyoyo za watu! Watu wenye mapenzi mema na uchungu kwa nchi yao wanasema, Dr. Magufuli, kaza uzi, wembe ni ule ule, ili nidhamu na uwajibikaji viweze kustawi na kushamiri miongoni mwa wafanyakazi wa umma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.