2016-12-08 14:43:00

Mshikamano wa Papa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Indonesia


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Alhamisi, tarehe 8 Desemba 2016 aliwageukia wananchi wa Kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia waliokumbwa na tetemeko la ardhi, Jumatano tarehe 7 Desemba 2016 na kusababisha watu zaidi ya 97 kufariki dunia na wengine 73 kupata majeraha makubwa kadiri ya taarifa za vyombo vya habari. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi; waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki; waliopatwa na majeraha pamoja na kupoteza makazi yao.

Baba Mtakatifu anawaombea nguvu na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki kigumu na aendelee kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu waliofukiwa na kifusi baada ya kuangukiwa na  majengo wakati wa tetemeko hilo! Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa makundi mbali mbali ya waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia. Kwa namna ya pekee, amewaombea wanachama wa Umoja wa Vijana Italia wanaorudia ahadi zao kwa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, ili aweze kuwaombea neema na baraka; ili kweli chama chao kiweze kuwa ni shule ya utakatifu na huduma ya ukarimu kwa Kanisa na ulimwengu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye katika kumtolea heshima Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili. Kwa njia hii, anataka kuonesha Ibada yake ya pekee kwa Mama wa Mungu na Kanisa. Mwishoni, anawatakia wote Siku kuu na safari njema ya Kipindi cha Majilio, daima wakiongozwa na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.