2016-12-07 12:26:00

Matumaini ni fadhila ya wadogo!


Mwenyezi Mungu anawatuliza na kuwaokoa watu wake, anawataka kumwandalia Mungu njia katika maisha yao, ili hatimaye, waweze kuuona utukufu wa Mungu. Kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 7 Desemba 2016 ameanza mfululizo wa Katekesi kuhusu matumaini ya Kikristo ambayo ni kiu ya wengi na kamwe hayawezi kumdanganya mtu, hasa nyakati hizi ambamo kuna watu wanakumbana na majanga mbali mbali ya maisha. Walimwengu wanahitaji cheche za matumaini ili kufukuzia mbali giza la maisha linaloendelea kuwaogofya watu.

Fadhila ya matumaini ni kielelezo makini cha uwepo wa Mungu anayefanya hija na watu wake, huku akiwashika mkono na kutembea nao bega kwa bega bila kuwaacha pweke! Yesu ameshinda ubaya wa dhambi na mauti na hivyo amewakirimia waamini maisha mapya. Kipindi cha Majilio ni wakati wa kumngoja Masiha, ni wakati wa kusubiri Fumbo la faraja kwa njia ya Umwilisho wa Neno wa Mungu, Mwanga wa Noeli. Nabii Isaya ni kati ya Manabii wakuu waliotabiri ujio wa Masiha ulimwenguni kwa kuwatangazia watu wa Mungu faraja itakayoletwa na Mkombozi atakapozaliwa na hivyo kukomesha kabisa mateso na mahangaiko kwa watu wake pamoja na msamaha wa dhambi unaoponya na kufariji moyo unaoteseka.

Nabii Isaya anawataka watu kumwandalia Mwenyezi Mungu njia na mapito Jangwani, ili awarejeshe tena kutoka utumwani Babiloni! Hii ni njia ya wokovu na ukombozi kutoka katika vikwazo vinavyoweza kuwakwamisha watu katika safari yao ya maisha. Waisraeli walipokuwa utumwani Misri walipoteza: Nchi, uhuru, utu, heshima na imani yao kwa Mwenyezi Mungu. Ni watu waliokuwa wanatangatanga pasi na matumaini.

Kumbe, mwaliko wa Nabii Isaya unafungua nyoyo kwa ajili ya matumaini mapya, kwa kutambua kwamba, Jangwani watakabiliwa na mapambano yak ufa na kupona, lakini huko ndiko ambako Mwenyezi Mungu amewaandalia njia na mapito, ili kuweza kuwa na matumaini na kicheko cha furaha, kama mtoto anaposubiria sahani ya wali! Kicheko cha furaha ni cheche za matumaini anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kicheko cha matumaini ya kukutana na Mwenyezi Mungu, kwa kujiaminisha kwake licha ya matatizo na changamoto mbali mbali za maisha. Watoto ni alama ya matumaini na kioo cha maisha. Ni katika mantiki hii, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho amejifanya kuwa mtoto na kuzaliwa na Bikira Maria.

Kama masharti ya kukutana na Mungu katika maisha, Yohane Mbatizaji alitoa mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ni changamoto pia kwa watu wa nyakati hizi kutubu na kumwongokea Mungu kwani kuna watu wengi wamekengeuka na kupoteza dira ya maisha na imani yao kwa Mungu aliye hai. Waamini watubu, ili kuweza kuiona njia ya maisha ya uzima wa milele iliyoandaliwa mbele yao, ili kukutana na Mtoto Yesu atakeywapatia tena kicheko cha furaha na matumaini.

Utumwa unawakandamiza watu hata katika nchi zao wenyewe kwa kuwakosesha mwamko wa kujisikia kuwa wako nyumbani. Mwenyezi Mungu anataka kuandika historia mpya maisha ya watu wake kwa kutembea pamoja na wao na wala si kama wafanyavyo wakuu wa mataifa! Hii ni historia ya uzima wa milele inayofumbwata na maisha ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa maneno machache anasema Baba Mtakatifu, hii ni historia inayoundwa na watu wadogo wanaowakilishwa na watu kama Mzee Zakaria na Elizabeth waliokuwa tayari na umri mkubwa licha ya ugumba wa Elizabeth.

Ni historia inayoandikwa na Bikira Maria, mchumba wake Mtakatifu Yosefu mtu wa haki; historia inayopambwa na uwepo wa wachungaji kondeni, watu waliokuwa wanaangaliwa kwa “jicho la kengeza” na kupuuzwa na jamii kwani hawakuwa ni mali kitu! Hawa ndio walionyanyuliwa juu na imani yao kama “Mlingoti wa bendera”, ili waendelee kuwa na matumaini kwani hii ni fadhila ya watu wadogo na wanyenyekevu wa moyo! Watu wadogo katika imani ndio wale wanaoleta mabadiliko katika maisha ya watu! Ni wale wanaogeuza Jangwa la utumwa, upweke, mahangaiko ya ndani na hali ya kukata tamaa, kutoka kifua mbele ili kukutana na utukufu wa Mungu, mwaliko kwa waamini kuacha nafasi katika nyoyo zao ili fadhila ya matumaini iweze kuchipuka katika majangwa ya nyoyo zao na kamwe matumaini hayawezi kumdanganya mtu awaye yote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.