2016-12-07 09:46:00

Endelezeni uzuri wa miji unaofumbata matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza washindi waliopewa tuzo maalum wakati wa mkutano wa pamoja wa taasisi zote za kipapa uliofanyika, Jumanne, tarehe 6 Desemba 2016 chini ya uongozi wa Kardinali Giafranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la utamaduni ambaye pia ni Rais wa Baraza la sanaa na utamaduni pamoja na Baraza la Kuratibu taasisi zote za kipapa. Washindi mbali mbali wanahimizwa na Baba Mtakatifu kuendeleza ari na moyo wa kufanya tafiti mbali mbali ili kutoa mwelekeo wa utu wa binadamu unaofumbatwa katika mwono wa Kikristo pamoja na kuendeleza upendo na urafiki kati ya watu.

Baba Mtakatifu anampongeza Professa Vitaliano Tiberia, aliyemaliza muda wake wa uongozi na kumkaribisha Professa Pio Baldi aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Rais mpya wa Taasisi ya Sanaa na fasihi ya Patheon, iliyoanzishwa kunako mwaka 1542, ambayo iliandaa tukio hili, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Cheche za uzuri kwa ajili ya uso wa binadamu mijini”. Hii ni tema ambayo inajadili kwa kina na mapana changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya watu kutokanana kukata tamaa kwa kukosa matumaini katika medani mbali mbali za maisha.

Hali hii pia inachangia mahusiano tenge kati ya watu, kiasi hata cha matendo ya kikatili kuongezeka na matokeo yake ni watu kujikatia tamaa. Kutokana na changamoto hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, wasanii wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira ya utulivu wa kijamii, kwa kuwapatia watu furaha inayobubujika kutoka katika uhalisia wa maisha yao, cheche ya faraja na matumaini.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maboresho ya maeneo ambayo yako pembezoni mwa miji, ili kuwapatia watu fursa za kustarehe katika maeneo ambayo yana mvuto wa uzuri, yanaheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu. Kabla ya kuporomoka kwa uzuri wa miji anasema Baba Mtakatifu, utu na thamani ya binadamu vinawekwa kwanza rehani. Leo hii, miji mingi inafumbata woga na wasi wasi, licha ya vijana kuwa na ndoto njema. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha mazingira bora zaidi, ili kuwajengea watu utamaduni wa kushangaa uzuri wa kazi ya uumbaji.

Baba Mtakatifu anawaalika wasanii na wajenzi kuhakikisha kwamba, wanachora majengo ya Makanisa yenye mvuto, hata katika hali yake ya kawaida pamoja na kuzingatia mambo msingi ambayo ni cheche za uzuri. Kwa njia hii, maeneo haya yanaweza kuwa pia ni chemchemi za uzuri, amani, ukarimu pamoja na kujenga mazingira bora zaidi yanayowawezesha waamini kukutana na Muumba wao sanjari na kujenga umoja na udugu na ndugu zao waamini na hivyo kuwa ni alama rejea ya ukuaji endelevu wa raia wote unaofumbatwa katika amani na mshikamano wa kijumuiya.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kweli cheche za upendo ziweze kuwaunganisha watu, maisha ya mjini na mazingira mambo ambayo wakati mwingine yanasigana kutokana na hali ya kutojali pamoja na ugumu wa moyo.

Hapa wasaniii wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kutoa cheche za uzuri wa Injili ya Kristo; matumaini na imani kwa watu waliokata tamaa kutokana na ubaya na jamii kutowajali wala kuwathamini. Wasanii katika medani mbali mbali za maisha, wawe ni cheche zinazofukuza giza la maisha ya watu; wawe ni watunzaji wa uzuri; watangazaji na mashuhuda wa matumaini kwa binadamu wote. Wasanii wanahimizwa kulinda na kutunza uzuri, ili kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu kutoka katika undani wake.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwatia moyo vijana wote wanaojihusisha na masuala ya sanaa, kusimama kidete, ili kuchangia kwa hali na mali ubinadamu unaofumbata mwono wa Kikristo. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumpatia “Tuzo ya Taasisi za Kipapa”  Dr. Chiara Bertoglio kutokana na mchango wake makini katika tafiti mintarafu muziki, fasihi andishi na masuala ya matamasha ya muziki. Mwingine ni Dr. Claudio Cianaglioni kwa utafiti wake wa kishairi kwa magwiji wa mashairi katika ulimwengu mamboleo, kati yao ni Padre David Maria Turoldo, ambaye jamii inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa.

Baba Mtakatifu ametoa pia Tuzo ya Kipapa kwa Dr. Michele Vannelli na Bwana Francesco Lorenzi kwa kutambua mchango wao katika masuala ya muziki. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote mafanikio mema katika masuala ya elimu, tafiti na huduma kwa familia ya Mungu. Amewaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, asiye na doa, cheche za uzuri wa Mungu anayemetameta kutokana na ulinzi wake wa kimama kwa waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku. Anawaomba wamkumbuke na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.