2016-12-06 10:00:00

Waswahili wekeni fedha zenu Benki, nyumbani zitaliwa na mchwa!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyingi majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki kuepusha kuhatarisha usalama wao.  Ametoa ushauri huo Jumatatu, Desemba 5, 2016 wakati akifungua tawi la Benki ya Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa. Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani si nzuri kwa sababu wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia benki mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha zao. Akizungumzia kuhusu kufunguliwa kwa tawi la benki ya Uchumi wilayani Karatu, Waziri Mkuu alisema unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo cha maendeleo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliushauri uongozi wa benki ya Uchumi kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata tija. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Wilson Ndesanjo alisema benki hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mtaji mdogo jambo linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika mikoa mingine.

“Changamoto nyingine ni baadhi ya wateja kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati, ambapo hatua za kisheria zikichukuliwa wanakimbilia mahakamani. Matukio haya yanadhoofisha kasi ya utoaji wa huduma kwani kesi zinachukua muda mrefu,”alisema. Bw. Ndesanjo alisema kuna baadhi ya kesi zimechukua miaka sita bila ya kumalizika hivyo kuzuia fedha ambazo kama zingerejeshwa kwa wakati zingezungushwa kwa wananchi wengine. Benki ya Uchumi ilianzishwa Septemba 22, 2005 ikiwa na mtaji wa sh. milioni 372. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016 mtaji huo umefikia sh. bilioni 5.4 hivyo umeongezeka mara 14.5 zaidi ya ule wa awali uliokuwepo wakati wa uanzishwaji wake.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia Mahongo kuhakikisha mashine zote za kupampu maji zilizoko ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo cha maji cha Qangded ziwe zimeondolewa ifikapo saa 12.00 jioni ya tarehe 5 Desemba 2016 na atakayekaidi amri hii atachukuliwe hatua za kisheria. Amesema kitendo cha kuweka mashine za kusukuma maji karibu na chanzo hicho na kuvuta maji kwenda kwenye mashamba yao kinasababisha maji kushindwa kufika katika mashamba ya wakulima wengine hivyo amewataka wafuate utaratibu uliowekwa na waendeshaji wa mradi huo.

Waziri Mkuu ametoa agizo Jumatatu, Desemba 5, 2016 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Jobaji kata ya Baray wilayani Karatu, ambapo amesema Serikali haitavumilia kuona mtu mmoja akivuruga mradi huo wa umwagiliaji. Amesema ili kuhakikisha mradi huo wa umwagiliaji unakuwa endelevu lazima chanzo cha maji kilindwe na wananchi wasiruhusiwe kufanya shughuli za kijamii karibu na chanzo na badala yake wasogee umbali wa mita 500.

"Sitaki kuona mashine zikipampu maji ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo na badala yake wakulima wote wafuate taratibu zilizowekwa . Lazima chanzo kilindwe kwa sababu maji yakikauka mazao nayo yatakauka, hivyo tutakosa chakula jambo ambalo hatutaki litokee. Mkuu wa wilaya kesho nenda kafanye ukaguzi katika chanzo ukikuta mashine kamata," amesema. Awali, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Jobaj unaotekelezwa na shirika la World Vision Tanzania uliogharimu sh. milioni 285. Mradi huo utahudumia vijiji vitatu vya Kata ya Baray ambavyo ni Mbunga Nyekundu, Jobaj na Dumbechand.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Wolrld Vision Tanzania, Bw. Revocutus Kamara amesema mradi huo unatokana na hitaji kubwa la maji katika vijiji hivyo vitatu na uwepo wa kisima kirefu cha maji kilichochimbwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2009. "Mradi huu wa maji unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Machi hadi Novemba 2016, ambapo wakazi 5,272 ikiwa ni pamoja na taasisi nne za Serikali ambazo ni Zahanati, Magereza, shule ya msingi na sekondari zilizoko katika kijiji cha Jobaj wananufaika kwa kupata maji safi na salama," amesema. Awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo itaanza Desemba 2016 na itagharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

Akizungumza kuhusu mradi wa umwagiliaji Mkurugenzi huyo amesema shirika lao limechangia kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga kilomita 1.716 za mfereji katika kijiji cha Jobaj (kilomita moja) na Dumbechand (mita 716) ambapo umegharimu zaidi ya sh. milioni 210 na inalenga kunufaisha zaidi ya wakulima 4,450 wa vijiji hivyo. Amesema mifereji hiyo itawezesha wakulima katika vijiji hivyo kuwa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya chakula na biashara hivyo itasaidia kupunguza migogoro ya maji, kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 803 hadi hekta 1,203.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.