2016-12-06 09:22:00

Kipaumbele cha kwanza: Uekumene wa damu, huduma na sala!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwa mwelekeo huu, mashuhuda wa imani, tayari wamekwisha jenga umoja wa Kanisa kwa njia ya kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani linaendelea na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani na wakati huu, maadhimisho haya yanafanyika mjini Strasbourg, Mashariki mwa mpaka wa Ufaransa na Ujerumani.  Huu ni mwendelezo wa maadhimisho haya yaliyozinduliwa mjini Lund, Sweden kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Mwaka 2016 unafungwa kwa kukazia zaidi Uekumene wa damu ambao ni hatua kubwa iliyokwisha fikiwa na Makanisa. Ni mwaka ambao Baba Mtakatifu Francisko amebahatika kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Kiorthodox kama Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Cyrill wa Moscow na Russia nzima.

Papa ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Lund pamoja na kushuhudia Tamko la Lund la Uekumene wa huduma kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Amefuatilia kwa ukaribu maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox huko Kisiwani Creta. Majadiliano ya kiekumene ni safari ndefu inayohitaji uvumilifu, udumifu na ushiriki mkamilifu. Kardinali Kurt Koch ana matumaini ya mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene hasa kutokana na jitahada kubwa zinazoshuhudiwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ilikuwa ni fursa ya kuangalia kwa moyo wa shukrani yale mema yaliyoibuliwa na mageuzi haya kama chachu ya mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili, ili kutoka katika kinzani na kuanza kuelekea katika ujenzi wa umoja wa Kanisa. Hii ni kumbu kumbu pia ya miaka 50 ya majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Matunda ya majadiliano haya yalijitokeza kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1999 kwa Makanisa kutia mkwaju katika Tamko la pamoja kuhusu “Kuhesabiwa haki ndani ya Kanisa”. Sasa mwelekeo ni kutoa tamko litakalowawezesha waamini wa Makanisa haya mawili kufanya toba, tayari kujikita katika upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Si wakati tena wa kuendekeza kinzani na migogoro ya kivita, badala yake waamini wajikite katika Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa jirani zao. Majadiliano ya kiekumene yanamwilishwa katika hija ya pamoja miongoni mwa Wakristo ili kuwa na lengo moja. Wakatoliki na Waluteri kwa sasa wanajiandaa kutoa tamko kuhusiana na “Kanisa, Ekaristi Takatifu na Utume”. Lakini, ikumbukwe kwamba, Makanisa yote yamebahatika kuwa na mashuhuda wa imani; watu waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kumbe, Uekumene wa damu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa ajili ya Makanisa yote. Hi damu ya mashuhuda wa imani, itakayokuwa mbegu ya umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.