2016-12-06 07:30:00

Kardinali Massaja alivyojisadaka kwa ajili ya Uinjilishaji Ethiopia!


Ushuhuda wa utakatifu wa maisha ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa waamini wote kwani una mvuto na mashiko kwa walimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia waamini 24 kutangazwa kuwa ni wenyeheri, kati yao waamini 23 waliuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani ya Kanisa Katoliki “Odium fidei”. Waamini nane wamewekwa kwenye orodha ya watumishi wa Mungu, tayari kuendeleza mchakato wa kutangazwa kuwa wenyeheri na hatimaye watakatifu kadiri ya mpango wa Mungu.

Mashuhuda hawa wa imani ni watu walioteseka na hatimaye kuuwawa kutokana na chuki za kiimani huko Hispania kwenye miaka ya 1936. Kardinali Guglielmo Massaja ametambuliwa kuwa na karama za ujasiri wa imani, uliomwezesha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatangazia wananchi wa Ethiopia Habari Njema ya Wokovu. Alizaliwa kunako mwaka 1809 huko Piovà d’Asti na wakati huo alijulikana kama Lorenzo Antonio Massaja, lakini alipoingia kwenye Shirika la Wakapuchini akachagua jina la Gugllielmo kama heshima kwa Paroko wake aliyemsaidia kugundua wito wa maisha ya kitawa.

Kunako mwaka 1832 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika maisha yake kama Padre akashuhudia utakatifu wa maisha, akaonesha unyenyekevu, ari na moyo mkuu katika utume wake, daima akiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Kunako mwaka 1846 Papa Gregori wa XVI akamteuwa kuwa Askofu na kumtuma kwenda Ethiopia ili kuanzisha Jimbo jipya. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa ya kimissionari, lakini akapiga moyo konde na kufunga vilago kuelekea Barani Afrika akiwa na umri wa miaka 36 tu.

Safari hii ilidumu miaka sita ya shida na taabu, akapambana na changamoto ya kiimani katika nchi kama Ethiopia iliyokuwa imejikita katika utamaduni wa Kikristo tangu kale. Askofu Massaja akajitaabisha kujifunza lugha ya wenyeji wake, tayari kujitamadunisha na kutamadunisha Injili ya Kristo ili iweze kupenya katika maisha ya watu, akafanikiwa kuandika Katekesimu ambayo ilikuwa ni muhtasari wa imani ya Kanisa, Sakramenti za Kanisa ambazo ni chemchemi ya maisha mapya katika Kristo, maisha adili yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Amri za Mungu na maisha ya sala kama kielelezo cha majadiliano kati ya Mungu na waja wake.

Katika maisha na utume wake, akajisadaka ili kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa haki na amani; chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu kwa kuthamini utu na heshima yao. Akasimama kidete kupambana kufa na kupona dhidi ya biashara haramu ya utumwa, uliokuwa unadhalilisha utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Akawasaidia wananchi kupambana na magonjwa, kiasi cha kupachikwa jina kuwa ni “Baba wa wagonjwa nchini Ethiopia”. Akafanikiwa kuanzisha Jimbo Katoliki la Addis Ababa, lakini hakufanikiwa kuona matunda ya kazi na utume wake mjini Addis Ababa kwani alipelekwa uhamishoni.

Kunako mwaka 1879 Mfalme Yohannes IV ili kuwafurahisha waamini wa Kanisa la Kikoptik, akamfukuza Askofu Massaja kutoka Ethiopia na hivyo kulazimika kung’atuka kutoka madarakani na kuliacha Jimbo lake likiwa wazi. Alipowasili nchini Italia, Papa Leo wa XIII kwa kutambua ushuhuda wake wa imani, mapendo na matumaini akamteuwa kuwa Kardinali na kuendelea kuchapa kazi za Uinjilishaji wa watu hadi alipofariki dunia kunako mwaka 1889 huko San Giorgio Cremano, nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.