2016-12-03 12:27:00

Jengeni mshikamano na maskini kwa kusikiliza na kujibu kilio chao!


Wafanyabiashara 400 waliokuwa wanashiriki katika Jukwaa la Majadiliano lililoandaliwa na “Fortune Time” lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Changamoto za Karne ya 21: ujenzi wa mafungamano ya kijamii”, Jumamosi, tarehe 3 Desemba 2016 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Papa amewapongeza kwa kujadili mada hii ambayo ni changamoto kubwa kwa nyakati hizi, ili kujenga mifumo ya uchumi shirikishi na inayojikita katika usawa! Hii imekuwa ni fursa kwa wafanyabiashara hawa kuweza kubadilisha mawazo na mang’amuzi mbali mbali ya maisha, ili kuhakikisha kwamba, changamoto hizi zinavaliwa njuga, ili watu wengi waweze kunufaika.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kusimama kidete kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu katika taasisi na kwenye mifumo mbali mbali ya uchumi, sanjari na kuonesha mshikamano wa pekee na maskini, wakimbizi na wahamiaji; makundi ambayo mara nyingi yanasahauliwa na Jamii. Kwa kutosikiliza kilio cha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni kuwanyima haki zao; kwa kutupilia mbali busara na hekima kiasi hata cha kushindwa kutumia karama na mapaji yao; mapokeo na tamaduni zao.

Kwa njia ya mtindo huu wa maisha, maskini wanateseka zaidi na wale waliobahatika kuwa na uwezo wa kiuchumi wanaendelea kunyongonyea katika umaskini: ki hali, kimaadili na kiroho! Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa amani na utulivu. Hali hii inasababishwa na ukosefu wa usawa kati ya Jamii tajiri na”akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, vita na umaskini pamoja na mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa makundi makubwa ya watu kujikuta yakikimbia au kuzihama nchi zao. Watu wanataka sauti zao ziweze kusikika ili hofu na matatizo yao yaweze kushughulikiwa pamoja na kunufaika na rasilimali na mchakato wa maendeleo ambao kwa bahati mbaya, unawafaidisha watu wachache ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mazingira kama haya yanapelekea kinzani na mipasuko inayofunua madonda makubwa, lakini kwa upande mwingine, inaweza kuwa ni nafasi ya kuwa na matumaini, kwa kutambua maovu yanayoisonga jamii ili kutafuta njia ya kuyaganga na kuyaponya. Kumbe, uwepo wa wafanyabiashara hawa ni alama ya matumaini kwa kutambua changamoto zilizoko mbele yao, tayari kuzivalia njuga ili kupyaisha matumaini yanayojikita katika wongofu wa kitaasisi na katika ngazi ya mtu binafsi; kwa kuguswa na utu, tamaduni, imani na mapokeo yao.

Wongofu huu anasema Baba Mtakatifu, si lazima sana ujikite katika soko la kiuchumi, uwiano mzuri wa mahesabu, maendeleo ya malighafi na maboresho ya miundombinu. Hapa kipaumbele cha kwanza ni utu wa binadamu, haki zake msingi, mgawanyo bora wa rasilimali ya dunia pamoja na fursa sawa zitakazowajengea watu uwezo wa kutumia kikamilifu nguvu iliyomo ndani mwao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ili kukabiliana na changamoto mamboleo za ukosefu wa haki msingi za binadamu kuna haja ya kuhakikisha kwamba, uchumi unakuwa ni shirikishi na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na jamii! Watu waguswe na mahangaiko ya jirani zao, hali inayohitaji upyaisho na uimarishaji wa mifumo ya kiuchumi inayofumbatwa katika wongofu binafsi na ukarimu kwa maskini!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wafanyabiashara hawa kuendeleza mchakato wa ugunduzi katika mifumo ya kiuchumi, ili kukidhi mahitaji na huduma kwa binadamu, hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wajumbe hawa wanahamasishwa kuwa ni msaada na sauti ya maskini, kwa kuwasikiliza na kujifunza kutoka kwao, ili kutambua na hatimaye, kujibu kilio cha shida na mahangaiko yao ya ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.