2016-12-02 07:03:00

Wasaidieni waamini kukutana na Uso wa huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa pia ni nafasi kwa wakuu na wahudumu wa madhabahu ya huruma ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za Italia, kukutana ili kutafakari dhamana n anafasi ya Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu; huruma inayopaswa kumwilishwa katika bararabara na mitaa ya waamini huko waliko, kielelezo cha imani tendaji. Askofu Tommaso Caputo, hivi karibuni kwenye Madhabahu ya Pompei alitumia nafasi hii kuwakaribisha wajumbe kwenye kongamano la 51 ya wahudumu wa madhabahu ya huruma ya Mungu nchini Italia, ili kuweza kukazia kwa mara nyingine tena huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya waamini, mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri katika mahubiri yake alikazia nafasi na dhamana ya Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu katika historia ya ukombozi. Ni Mama ambaye ameonesha: huruma, mapendo na hujaji wa imani pamoja na waamini na watu wote wenye mapenzi mema, walioandamana pamoja naye, huku akiwahakikishia wale wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu matumaini yasiyodanganya kamwe!

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wale wote wanaobahatika kuingia kwenye madhabahu ya huruma ya Mungu wanaonja huruma na mapendo ya Mungu katika maisha yao. Iwe kwao ni nafasi ya kukutana na Uso wa huruma ya Mungu, yaani Kristo Yesu kwa njia ya Neno na Sakramenti zake; kwa njia ya huduma makini, ukarimu na upendo. Ni wajibu wa Kanisa kuhakikisha kwamba, madhabahu yanakuwa ni kielelezo cha imani, huruma na mapendo ya Mungu kwa waja wake. Madhabahu haya yawe ni mahali pa ukimya, sala, tafakari, upendo na upatanisho kati ya Mungu na jirani. Hata wale wanaoteseka katika hali ya upweke, magonjwa na kukata tamaa, waonje ndani mwao upendo wa Mungu unaokoa na kuponya.

Kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, watu waonje matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watambue kwamba, shida, mahangaiko, matatizo na changamoto zao za maisha hazina neno la mwisho katika maisha yao, bali Mwenyezi Mungu ndiye anayeongoza historia na maisha ya mwanadamu! Madhabahu yawe ni mahali pa kuonja: huruma, upendo, upatanisho na mahali pa kupyaisha imani ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji! Waamini wawe na ujasiri wa kusimama na kutembea kifua mbele kwa imani, matumaini na ujasiri bila woga wala mashaka kwani Kristo Yesu ameshinda dhambi, kifo na mauti, chachu ya matumaini mapya!

Mwanadamu hapa duniani anasema Kardinali Beniamino Stella daima yuko kwenye mapambano ya maisha, yanayofumbata furaha, huzuni, majonzi na hata wakati mwingine hali ya kukata tamaa na kuanguka kwenye ombwe la maisha. Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, hata katika hali na mazingira kama haya, Mwenyezi Mungu bado anafanya hija na watu wake katika historia na maisha yao ya kila siku, jambo la msingi ni kuwa na imani, matumaini na mapendo, kwani Mwenyezi Mungu anataka kukutana nao ili aweze kuwaokoa. Huu ni mwaliko wa kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake, ili kumwachia nafasi, aweze kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wake kama alivyofanya Kristo Yesu kwa kujisadaka bila ya kujiachilia hata kidogo; kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano.

Madhabahu yawe ni mahali pa kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma na upendo wa Mungu ni kiini cha Injili, pasi na mambo haya makuu, imani ingekosa utamu na uzuri wake wa kujisadaka kwa ajili ya wengine, ili kuonja huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha ya kila siku. Kardinali Stella anakaza kusema, Upatanisho ni kati ya mang’amuzi mazito ambayo mwamini anayejitaabisha kufanya hija ya maisha yake ya kiroho anapenda kuonja akiwa kwenye Madhabahu. Hapa ni mahali anapoonja ule ukimya wa ndani, anapogusa undani wa maisha yake yaani utakatifu na madhaifu yake, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu.

Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti ya Upatanisho ni chakula muhimu sana kwa mahujaji wanapotembelea Madhabahu ya huruma ya Mungu. Maadhimisho haya yanarejesha tena furaha ya maisha ya kiroho, kwa kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu. Mwenyezi Mungu anatua mizigo ya waja wake na kubomolea mbali kuta za ubinafsi, uchoyo, kiburi na hali ya kutojali wengine. Uso wa huruma ya Mungu una nguvu ya kuwainua tena wale walioanguka dhambini, tayari kuendelea na mapambano ya maisha ya kiroho kwa ari na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.