2016-12-02 10:37:00

Mtayarishieni Bwana mapito yake!


Kipindi cha Majilio ni wakati wa kungojea, ni wakati ambao unafanana na hali wanayokuwa nayo familia fulani au jamii fulani wanapomngojea mgeni ambaye amewaahidi kuwajia. Mazingira yatawekwa safi, maandalizi ya chakula na vinywaji yatafanyika na bila kusahau maandalizi binafsi ya kifikra kwa ajili ya ujio huo. Sisi waamini tumetaarifiwa ujio huo na mzaburi anapotuambia kwamba: “Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye Bwana atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu”.

Masiha huyu ambaye tunamngojea ujio wake anaelezewa kinagaubaga katika somo la kwanza na yale tutakayonufaika nayo. Nabii Isaya anamtaja Yeye ambaye atatoka katika shina la Yese ndiye huyu anayekuja, ndiye huyu tunayemngojea na anatuletea upya wa maisha kwa njia ya mapaji ya Roho Mtakatifu. Mzaburi anamtaja Roho Mtakatifu kama mpyaishaji wa uso wa dunia: “Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi” (Zab 104: 30). Yeye anayejazwa Roho Mtakatifu “hutenda matendo makuu ya Mungu” (Rej. Mdo 2:11). Hivi ndivyo Nabii Isaya anavyomfafanua huyu anayetoka katika shina la Yese aliyejazwa mapaji ya Roho Mtakatifu ambayo ni vipaji vya kimbingu yanayouletea ulimwengu huu wokovu,  na kuuelekeza ulimwengu  kurudi katika namna yake ya asili tangu uumbwaji wake.

Ujio huu wa Masiha kwa hakika unatuletea wokovu. Je, ni wokovu  wa namna gani? Kile kinachookolewa huwa kinaepushwa na hali mbaya na kuingizwa katika hali njema. Tunapoendelea kulitafakari somo la kwanza la Dominika hii hali hiyo njema inaonekana. Amani na uelewano inatawala kati ya viumbe vyote, hukumu za haki na maonyo katika unyenyekevu ndivyo vitashuhudiwa na yule mwovu ataondoshwa katika jamii yetu. Masiha anakuja kutuletea hali njema, anakuja kutuondoa katika uhasama, chuki, uadui, mafarakano kwani wakati wa ujio wake viumbe vyote “hawatadhuru wala hawataharibu ... maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari”.

Hivyo, ujumbe anaokuja nao Masiha si mwingine bali ni kuustawisha utawala wa Mungu kwetu. Hamu na matayarisho yetu yanapaswa kulenga katika hilo. Majira haya ya kungojea si ya kujitayarisha kwa kumshangaa au kumstaajabia huyo anayekuja bali ni matayarisho ya ndani ya mioyo yetu ambayo yatamwandalia njia huyo anayekuja ili kuipyaisha mioyo yetu na kutujaza huyu Roho wake kusudi nasi tuweze kusema matendo makuu ya Mungu. “Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake”. Mwaliko huu tunaousikia kupitia Yohane Mbatizaji unatupatia wajibu mahsusi wa kipindi hiki cha kungojea: “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake”. Matayayarisho yetu yatapata nguvu pale tutakapokuwa tayari kuzitambua hizo njia za Bwana na mapito yake yanapitia wapi. Ni wapi ambapo Bwana anataka kupita au ni nini ambacho Bwana anataka tumwandalie?

Yohane Mbatizaji anaendelea kutuonesha njia hiyo ni ipi na namna ya kuitayarisha. Njia hiyo ya Masiha ni mienendo yangu mimi na wewe katika maisha. Ni mwaliko kwetu sisi kungojea kwa kutafakari mienendo yetu ya maisha kama inakidhi kumpitisha Masiha ambaye amefafanuliwa vema katika somo ya kwanza hapo juu. Masadukayo na Mafarisayo hawa wanaweza kuonekana ndani ya nafsi yangu mimi na wewe, pale tunapojiona kuwa wajuzi zaidi na kujivika utawala wa ukweli wote au pale tunapojiona kuwa tu wema na tunaoshika dini na taratibu za kijamii zaidi ya wengine, na matokeo yake badala ya kujiandaa vema tukajikuta tunakabiliwa na adhabu ya Mungu kwani “pepeto lake li mkononi mwake”.

Hivyo, Yohane Mbatizaji anatuonya juu ya matayarisho yenye toba, matayarisho yenye kuwa na nia ya kubadili mienendo yetu. Kipindi hiki pia ni kipindi cha toba: “Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba”. Mabadiliko hayo ya ndani yaletwayo na toba ndiyo kadi pekee ya mwaliko wa kushiriki furaha itakayoletwa na Masiha. Pale tutakapokataa kushiriki katika matayarisho hayo kwa toba basi tutaikosa furaha hiyo. Yeye Masiha atakapokuja “atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika”. Basi ni wajibu wetu sisi kujiuliza kama tu  tayari kiasi gani na tutawekwa upande gani: ngano au makapi.

Matayarisho yetu pia yanataadharishwa na uwepo wa mazoea fulani fulani ya kiulimwengu. Ipo hatari ya kufikiri katika mrengo wa kidunia na kujiandaa kama wafanyavyo walimwengu. Ulimwengu umetusonga kiasi cha kujikuta mara nyingi tunajisahau kuyafanya yale matayarisho ya ndani na kujikita zaidi katika matayarisho ya nje nje tu. Tunadhani kwamba kuwa wakristo tu kwa ubatizo inatosha, hatujishughulishi na kuufanya huo ukristo ukue na kukomaa na matokeo yake hata yale yanapaswa kuchagizwa na ukristo huo yanakurupushwa. “Wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye Baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia Mungu anaweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto”.

Hiki ni kipindi cha kufanya tena tathimini ya namna ambavyo ninamwandalia Masiha njia katika mwenedo wangu wa maisha ya kila siku; namna gani ambavyo ninamfunua katika upendo wangu kwa jirani zangu; namna gani ninamtangaza kwa maneno yangu kwa jirani zangu, maneno ambayo yanatia nguvu, yanabariki, yanafariji na siyo maneno ambayo yanalaani na kusengenya; ni namna gani ninavyojenga madaraja na sio kuta katika mahusiano na wenzangu iwe ndani ya familia, katika jamii inayonizunguka na ulimwengu mzima. Namna hizo na nyingine nyingi ambazo hutokana na Roho Mtakatifu ndizo zinazomtengezea Masiha njia na kumtayarishia mapito yake. Bwana anakuja kutukomboa watu wake, anakuja kuturudishia tena hadhi yetu ambayo imechakaa kutokana na dhambi. Tukiwa katika kipindi hiki cha Majilio tumngojee kwa: imani, matumaini, mapendo na matendo ya toba na wongofu wa ndani.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.