2016-12-02 14:36:00

Jubilei ya Miaka 400 ya Waskolopi iwe ni Pentekoste mpya katika elimu!


Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, tarehe 27 Novemba 2016 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya mchakato wa kuzindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Calasanziani itakayofikia kilele chake hapo tarehe 25 Novemba 2017. Kwa waamini wote watakaotimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya wataweza kupata rehema kamili zinazotolewa na Baba Mtakatifu kadiri ya sheria za Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya amemtumia ujumbe mkuu wa Shirika la Waskolopi, Mheshimiwa Padre Pedro Aguado Cuesta, akiwapongeza kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 400 tangu Shirika lao lilipoanzishwa na miaka 250 tangu Mtakatifu Giuseppe Calasanzio alipotangazwa kuwa Mtakatifu kwa kuwataka kuendelea kuwa ni mashuhuda wa matumaini kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma kwa jirani, hasa watoto wadogo wanaohitaji elimu na malezi bora, ili kweli Jamii iweze kufanya mageuzi yanayojikita katika tunu msingi za Kiinjili zinazopaswa kutangazwa na kushuhudia hadi miisho ya dunia.

Ni Roho Mtakatifu aliyemwongoza Padre Giuseppe Calasanzio kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya elimu kwa watoto wadogo waliokuwa wanatangaza tanga kwenye mitaa na barabara za mji wa Roma pasi na dira wala mwelekeo wa maisha. Akawachagua Watawa wa Shirika la Watawa wa Paolini wa Mama maskini wa Mungu kumsaidia katika utume huu. Shirika hili likawa la kwanza duniani, kujitosa kimasomaso kwa ajili ya elimu kwa watoto na vijana hasa maskini na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Papa Pio XII akatambua mchango mkubwa wa Shirika hili na kumtangaza kuwa Mwenyeheri wakati wa kumbukumbu ya miaka 300 tangu alipofariki dunia na kumteua kuwa ni Msimamizi wa shule zote za Kikristo duniani. Tangu wakati huo, Shirika limejielekeza zaidi katika huduma ya elimu ndani na nje ya Italia; kwa kuwafunda watoto na vijana tunu msingi za maisha ya Kikristo: kiroho, kiimani na kimaadili pamoja na kuliwezesha Shirika kumwilisha karama yake katika medani mbali mbali za maisha ya watu; kwa kusoma alama za nyakati sanjari na kutekeleza shughuli mbali mbali za kichungaji kadiri ya mahitaji ya Kanisa.

Kutokana na changamoto ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Shirika likajielekeza zaidi katika mchakato wa kuwashirikisha zaidi waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na huo ukawa ni mwanzo wa Udugu wa Waskolopi wanaoshirikishana na watawa hawa: karama na utume wao kielelezo cha wingi wa zawadi ya miito kutoka kwa Roho Mtakatifu. Shirika lilianzishwa kunako mwaka 1597, ikapita takribani miaka 20 ndipo utambulisho wa Shirika ukaanza kuonekana, changamoto kwa maadhimisho ya Jubilei hii kuwa jinsi walivyo na kuendelea kutekeleza wito wao ndani ya Kanisa kwa ajili ya huduma ya elimu kwa watoto na vijana.

Jubilei hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, iwe ni “Pentekoste mpya” yaani mwanzo mpya, utakaowawezesha kuvuka vizingiti, kinzani, woga na wasi wasi wa kila aina ili kuwatangazia na kuwashirikisha watu wa Mataifa nguvu ya Injili inayookoa daima wakiwa na ari na moyo wa kimissionari, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Elimisha, Tangaza na Badilisha”, daima wakiwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ili kuwa kweli ni vyombo vya matumaini kwa watoto na vijana wanaowahudumia, ili kuleta mageuzi katika nyoyo za watu mintarafu Ufalme wa Mungu. Elimu iwe ni fursa kwa watu kuweza kumfungulia Mungu malango ya maisha yao, kwa kuwakirimia ujuzi na maarifa ili kuweza kusimika maisha yao katika nguzo ya upendo.

Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa hawa kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto na vijana ambao hawana fursa ya kwenda shule na wanatengwa na jamii kutokana na ubinafsi; kinzani na misigano ya kibinadamu; vita na migogoro ya kisiasa, kidini na kikabila; wote hawa wanahitaji kukutana na walezi bora na makini watakaowasaidia kukua na kusimika mizizi ya maisha yao kwa Kristo Yesu, anayewasindikiza katika safari yao ya maisha.

Huu ni utume wanaopaswa kuutekeleza kwa njia ya unyenyekevu, kwa kutambua kwamba wao ni maskini wanaowahudumia maskini, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyejinyenyekesha na kujitwalia hali ya ubinadamu, akazaliwa, akateswa na kufa Msalabani. Watambue kwamba, wanapaswa kuhudumia na wala si kuhudumiwa, ili kutoa mwanga wa matumaini kwa watoto na vijana wanaowazunguka. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kupata furaha na utimilifu wa maisha yao wanapowahudumia watoto wadogo, kwa kuwa maskini kwa ajili ya maskini na watoto kwa ajili ya watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.