2016-12-02 07:25:00

Comece na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya!


Maaskofu wawili wawakilishi wa Kamati ya Maaskofu Barani Ulaya, wameshiriki katika kikao cha viongozi wa dini na kamati ya Umoja wa Ulaya, kuhusu ushirikishaji, wakimbizi na tunu za Ulaya kwa maneno na matendo, kikao kilichofanyika tarehe 29 Novemba 2016, jijini Brussels, nchini Ubelgiji. Monsinyo Jean Kockerols, Mwenyekiti msaidizi mstaafu wa Kamati ya Maaskofu Barani Ulaya, amewasilisha uhalisia wa mambo na ushiriki wa Kanisa Katoliki Ulaya katika kushughulikia wahamiaji. Amesema kwamba, changamoto hiyo ya wahamiaji imeutikisa umoja na mshikamano wa dira na dhamira katika nchi za Ulaya, na hata Kanisa Barani Ulaya. Hilo linaonekana wazi, kwa jinsi ambavyo jumuiya za Kikristo zinavyokabiliana na changamoto hiyo katika maisha ya kila siku.

Askofu msaidizi wa Malines-Brussels kaelezea pia jinsi juhudi zinavyowekwa na makanisa mahalia katika kuwapokea wahamiaji na kuwafanya kuwa sehemu ya jamii kwa mipango ya muda mrefu, na hili linatokana na utambuzi wa dini kwamba ukarimu ni sehemu ya maisha ya mkristo. Suluhu ya pamoja juu ya wahamiaji na wakimbizi, inagusa moja kwa moja tunu msingi na maisha ya Ulaya kwa siku za usoni.

Monsinyo Czeslaw Kozon, Mwenyekiti msaidizi wa Kamati ya Maaskofu Barani Ulaya kaelezea mtazamo wa nchi za Scandinavia kwamba, ni muhimu kuzingatia umoja na mshikamano wa kifamilia katika kukabiliana na changamoto ya wahamiaji. Kila mmoja anayo haki ya kutengeneza familia, na wanafamilia wote wanayo haki ya kuishi pamoja. Kwa upande wa Askofu wa Copenhagen, kasisitiza heshima kwa uhuru wa kuabudu katika harakati za kuwapokea na kuwashirikisha katika jamii wahamiaji na wakimbizi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.