2016-12-02 14:23:00

Siku ya Kimataifa ya kukomesha biashara haramu ya utumwa


Ni  siku iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa tangu 2 Desemba 1949 .Ni siku muhimu kwasababu tarehe kama hiyo  Baraza Kuu liliridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kukomesha biashara  haramu ya binadamu.

Naye Padre Giulio Albanese mmisionari wa shirika la wakomboniani akihojiwa na waandishi wa habari wa Radio Vatican alisema ya kwamba katika biashara ya utumwa ni pamoja na  utandawazi uliopo duniani , na kuleta mateso makubwa ya binadamu na hasa kwa kizazi kipya  cha vijana ambao wamekuwa dhabihu altareni kwa sababu ya ubinafsi wa binadamu.

Alizitaja nchi kama Mauritania ambayo imekuwa na biashara ya utumwa kwa miaka mingi na nchi nyingine za Afrika kama vile Sudan, Benin na Mali; bila kusahahu baadhi ya nchi za kiarabu  kwa bahati mbaya alisema, wageni wanaishi hali isiyo ya kibinadamu ambapo ulazimishwa kufanya kazi kuanzia asubuhi hadi usiku.Kwa ujumla ni mateso yanayo athiri  watoto wadogo kulazimishwa kazi na kukosa haki msingi za binadamu   katika nchi za kusini mwa jangawa la sahara.

Na vilevile ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa katika siku ya  kimataifa ya kukomesha utumwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema mafanikio ya ajenda ya 2030 yenye kipengele cha kutokomeza utumwa mamboleo hayamo katika sheria bali yamo katika kupambana na sababu ya mizizi yake.Alisema wakati huu ni wa kukumbuka waathirika duniani kote na kutafakari mafanikio yaliyopatikana katika kuondoa aina zote za utumwa mamboleo, kama vile kazi za kulazimishwa, aina mbaya zaidi ya ajira ya watoto, ndoa za kulazimishwa na za utumishi, kazi za kitumwa na biashara haramu ya binadamu.

Aliongeza kuwa wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto, watu wenye asili ya Afrika, watu wa asili na wale wenye ulemavu, ambao mara nyingi hukabiliwa na unyonyaji na unyanyasaji. Vile vile alisema ongezeko la hivi karibuni la sheria zenye kuwaadhibu wale wanaokimbia vita na hali mbaya katika nchi zao vimechochea biashara ya utumwa na ulanguzi wa binadamu.

Hivyo Ban Ki Moon alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na wafadhili kuchangia katika mfuko wa hiari wa Umoja wa Mataifa, pamoja na kuwekeza katika miradi ya vituo vya usaidizi, ili kurejesha haki za binadamu na heshima ya maelfu ya waathirika na familia zao.Maadhimisho ya mwaka huu yamekwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 90 ya mkataba wa utumwa, pamoja na miaka 60 ya mkataba wa kukomesha utumwa, biashara ya utumwa, taasisi na zoezi la utumwa.

Na idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.