2016-12-01 07:12:00

Shuhuda wa Neno na Ukarimu wa Mungu kwa waja wake!


Utume wa Padre Andrea Santoro ulikuwa daraja na dirisha kati ya Kanisa la Roma na wakristo wa mashariki, mahali ambapo mitume Petro na Paulo walitokea kwenda kuitangaza Injili ya Kristo maeneo ya Roma. Padre huyu aliwasha cheche za moto wa Neno la Mungu na ukarimu katika jumuiya aliyoihudumia, akiwa zawadi ya imani, Fidei donum, kwa Kanisa la Uturuki, yeye akiwa Padre kutoka jimbo la Roma. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ndivyo anavyoelezea utume wa Padre Santoro, alivyoshuhudia Neno la Mungu na ukarimu mpaka siku alipouwawa mnamo tarehe 5 Februari 2006.

Kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka kumi, chama chenye jina la Padre Santoro wakishirikiana na jimbo la Roma, kimeandaa maonesho na shughuli mbali mbali kwa ajili ya kumkumbuka Padre Santoro na huduma yake kwa Kanisa la mashariki. Kumbukumbu hizo zimehitimishwa kwa adhimisho la Misa Takatifu lililoongozwa na Kardinali Sandri, Jumapili tarehe 27 Novemba, katika Kanisa kuu la Msalaba Mtakatifu wa Yerusalemu. Wakati wa mahubiri, Kardinali Sandri ameelezea namna gani Padre Santoro, baada ya kutoa huduma katika parokia za Roma, alisikia wito wa kuhudumia wakristo wa mashariki, maeneo ambapo kutoka kwayo Injili ilifika Roma, lakini sasa ni maeneo yanaoishi katika nyanyaso na dhuluma za uhuru wa kuabudu.

Mauaji ya mtu mwenye imani thabiti na shahidi wa Injili, Padre Andrea Santoro, yamekuwa jeraha kubwa kwa jimbo la Roma na Vikarieti ya kitume ya Anatolia.  Lakini ni jeraha ambalo leo linaonekana kuzaa matunda mengi ya kiroho. Padre Santoro alitambua uwepo wa roho waovu wenye kunuia mabaya, ndiyo sababu katika Biblia yake, alikuwa na kijitabu chenye sala ya kufukuza shetani na pepo waovu, kijitabu kilichoandikwa na Baba Mtakatifu Leo XIII. Hivi ndivyo alivyowasha mshumaa wa sala na matendo mema katika maisha yake. Kardinali Sandri anawaalika waamini kuiga mfano huo ili kuepukana na vishawishi vya shetani.

Mateso, nyanyaso, uonevu na vishawishi vyote vya dhambi vitashindwa iwapo waamini watabaki waaminifu kwa Kristo. Kama alivyofundisha katika kongamano la kumbukumbu ya miaka 100 ya Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kongamano lililoitwa, Damasko mche wa matumaini, Kardinali Sandri anasisitiza umuhimu wa kuweka juhudi katika elimu na malezi ili watoto na vijana wa mashariki waweze kuona tena mwanga wa matumaini katika nchi zao. Pamoja na ukweli kwamba miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kinzani na machafuko katika nchi za mashariki, waamini wanaalikwa kuwa kama wazee wenye ndoto za kuwasaidia vijana kuwa na maono ya maisha bora ya baadae. Ziendelee kufanyika juhudi za utafutaji amani kwa njia ya majadiliano, mazungumzano, elimu na malezi bora.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.