2016-12-01 14:44:00

Papa Francisko anaishukuru familia ya Mungu nchini Giorgia!


Ujumbe wa Kanisa Katoliki kutoka Georgia, Alhamisi, tarehe 1 Desemba 2016 umemtembelea Baba Mtakatifu Francisko kama alama ya shukurani kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyetembelea nchini mwao hivi karibuni. Huko aliweza kujionea mwenyewe tamaduni, tasaufi na familia ya Mungu iliyokuwa inamsifu na kumtukuza Mungu na Yesu Kristo Mwanaye wa pekee, Mkombozi wa ulimwengu pamoja na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu Francisko amewaushukuru ujumbe huu na kwa namna ya pekee, amekumbuka fadhila alizotendewa na Patriaki Elia wa pili, ambaye alimtambua kuwa kweli ni mtu wa Mungu kutokana na maisha yake. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, huko Georgia bado kuna matatizo na changamoto mbali mbali za maisha, lakini pia kuna cheche za matumaini na kwamba, mambo yatakwenda vyema bila kulazimisha kitu kwani pole pole ndio mwendo!

Baba Mtakatifu anakumbuka kwa moyo wa shukrani mkutano wake, maswali waliyomuuliza waamini walei na kwamba, aliona na kushuhudia mwenyewe utendaji na uwajibikaji wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Alibahatika kukutana na kuonana na wakleri, watawa na watu wenye mapenzi mema! Hili ni tukio ambalo kweli anapenda kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kutembelea Georgia na sasa anawashukuru wao kwa niaba ya familia ya Mungu kutoka Georgia. Kazi hii ni sawa na chachu ambayo itachachua maisha ya Kikristo ili yaweze kukua na kuchanua kama “mtende wa Lebanoni” kwa wakati wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwaomba wajumbe hawa kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.