2016-12-01 15:05:00

Mwachieni Mungu nafasi ili awapatie neema ya kutubu na kuongoka!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Alhamisi tarehe 1 Desemba 2016 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, amewataka waamini kuomba neema ya unyenyekevu ili waweze kujitambua kuwa ni wadhambi na wanahitaji kuonjeshwa na Mwenyezi Mungu huruma na msamaha, ili kutubu na kumwongokea Mungu hasa wakati huu wa Kipindi cha Majilio. Neema ya Mungu iwawezeshe waamini kushinda ubaya wa dhambi kwa kudhani kwamba, wanatenda mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama ilivyokuwa wakati wa kijana Saul aliyelitesa na kulidhulumu Kanisa la Kristo kwa kudhani kwamba, alikuwa anatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Kijana Saul alipokutana na Kristo Mfufuka, akatubu na kumwongokea Mungu. Hii inaonesha kwamba, binadamu wote ni wadhambi wanahitaji neema ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kuna waamini wanaoonesha shingo ngumu kwa kujificha anasema Baba Mtakatifu Francisko, hatari kwa ukuaji wa maisha ya mtu kiroho. Hapa kuna haja ya kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwatakasa, hizi ndizo shutuma ambazo Stefano shahidi alizitoa kwa wakuu wa Makuhani waliokuwa wanapingana na Roho Mtakatifu. Katika mawazo na nia yao, walionekana kana kwamba, wanatafuta utukufu wa Mungu, hali ambayo ilimgharimu Stefano, maisha, akawa ni shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Ukakasi wa maisha ya kiroho anasema Baba Mtakatifu ni kikwazo cha mchakato wa toba na wongofu wa ndani kinachomwaminisha mwamini kiasi cha kusahau uwepo wa Mungu katika maisha yake, mbegu ya dhambi inayopandikizwa na Shetani katika maisha ya waamini. Shetani anataka kukwamisha mchakato wa utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo. Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, lazima wamshuhudie Mungu kwa maneno na matendo yao, vinginevyo siku ya mwisho watakiona kilichomnyoa Kanga manyoya kwa kushindwa kuingia katika Ufalme wa Mungu.

Wakristo wanapaswa kuepuka mtego wa Shetani anayewapelekea daima kutaka kujisafisha na kuonekana watu wema mbele ya Mungu, lakini kumbe, wanateleza na kuangukia kwenye mtego wa Shetani. Neno la Mungu liwe ni nguzo na msingi thabiti katika maisha ya waamini, tayari kutubu na kumwongokea Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtoza ushuru aliyejisikia kuwa mdhambi na Farisayo aliyejiaminisha kuwa ni mwenye haki na mtenda mema akakosa baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya sala yake ya kujikweza na kujitukuza!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya maisha yao, ili aweze kuwakirimia neema na baraka ili kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuchukua Msalaba na kuendeleza safari ya ukombozi. Mahali ambapo yupo Kristo Yesu, hapo hapatakosekana Msalaba anasema Baba Mtakatifu: Msalaba ni kielelezo cha hekima, huruma na ukombozi kwa mwanadamu. Waamini wawe na ujasiri wa kujitambua kuwa ni wadhambi na wanahitaji neema ya kutubu na kumwongokea Mungu na kamwe wasimwekee Mungu kizingiti na hivyo kuendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi. Tafakari hii iwasaidie kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, yaani Noeli ya Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.