2016-11-30 15:27:00

Siku kuu ya Mt. Andrea Mtume: kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, mtume, mdogo wake Mtakatifu Petro mtume. Ni siku muhimu sana inayokuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ambalo linaadhimish Sherehe ya Mtume Andrea kwa kishindo huko Istanbul, Uturuki. Ujumbe wa Vatican katika maadhimisho unaongozwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo ambao umeungana pia na Askofu mkuu Paul F. Russell, Balozi wa Vatican nchini Uturuki.

Baada ya maadhimisho ya Liturujia Takatifu iliyoongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopoli, Kardinali Kurt Koch amewasilisha ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko uliokazia kwa namna ya pekee, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaoendelea kutekelezwa miongoni mwa Makanisa haya mawili, hadi pale, Mwenyezi Mungu atakapoamua kuyaunganisha Makanisa haya kuwa moja kwa kushirikiana katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hii ni changamoto kutoka kwa Mitume wasimamizi wa Makanisa haya pamoja na mashuhuda wa imani ambao kwa nyakati zote wamejifungamanisha na Kristo Yesu kiasi hata cha kuyamimina maisha yao, licha ya migawanyiko na utengano miongoni mwa Wakristo!

Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa la Kiorthodox kwa kuadhimisha Mkutano mkuu hapo Juni 2016 huko Crete kwa kudhamiria kuwaunganisha Wakristo wote. Licha ya utamaduni wa kale unaoyaunganisha Makanisa haya, lakini daima, kumekuwepo na matatizo na changamoto za ujenzi wa umoja wa Wakristo, mwaliko wa kuendeleza mchakato wa Wakristo kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi. Kumbu kumbu ya mahusiano na mafungamano ya Wakristo yamevurugwa kutokana na vita na kinzani zinazoendelea sehemu mbali mbali za dunia. Ni kwa njia ya sala, matendo ya huruma na majadiliano yatakayowawezesha Wakristo kuvunjilia mbali kuta za utengano na kuanza kushirikiana na kushikamana kama ndugu wamoja.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Wakatoliki na Waorthodox ambao umesaidia sana waamini hawa kutambuana na kuheshimiana kama ndugu, kwa kuheshimu karama za Makanisa haya na kwa pamoja wameshikamana ili kutangaza na kushuhudia Injili; kutoa huduma kwa binadamu pamoja na kuendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha: amani, utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, majadiliano ya kitaalimungu kati ya Makanisa haya mawili yameendelea kuchangia uelewano mzuri kati ya Makanisa haya mawili. Waraka wa pamoja  kuhusu “Sinodi na Ukuu wa Petro Karne ya kwanza; Kuelekea Uelewa wa pamoja katika Umoja wa Kanisa” ni matunda ya safari ndefu ya majadiliano ya kiekumene iliyotekelezwa na Kamati ya pamoja ya wanataalimungu wa Makanisa haya. Bado kuna mambo mengi anasema Baba Mtakatifu yanayopaswa kufanyiwa tafakari ya kina, lakini “Sinodi” na “Ukuu wa Petro karne ya kwanza” inaweza kuwa ni msingi unaoelekeza jinsi ya Ukuu unavyopaswa kutekelezwa ndani ya Kanisa wakati ambapo Makanisa ya Mashariki na Magharibi yatakapokuwa yamejipatanisha na kuungana kuwa ni Kanisa moja!

Baba Mtakatifu anakumbusha kwa moyo wa shukrani, mkutano wao huko Assisi uliowawezesha kukutana na kusali na Wakristo pamoja na wawakilishi wa dini mbali mbali duniani kwa ajili ya kuombea amani duniani. Hili lilikuwa ni tukio la furaha lililosaidia kuboresha urafiki unaofumbatwa kwa kuwa na mwono wa masuala yanayogusa maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, haya ni kati ya mambo ambayo alipenda kushirikishana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika ari na moyo wa udugu na kwamba, anamkumbuka daima katika sala na sadaka yake. Anamtakia amani, afya njema na baraka tele  kwake binafsi na kwa waamini anaowaongoza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.