2016-11-30 14:47:00

Kuombea wazima na wafu; Kuzika wafu ni sehemu ya matendo ya huruma!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa waamini kuweza kutafakari kwa kina na mapana matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kuombea walio hai na marehemu ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho. Maandiko Matakatifu yanasema “Bali tukitarajia kitu tusichokiona, twakingongea kwa saburi. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye achunguzaye nyoyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano, tarehe 30 Novemba 2016 iliyofunga rasmi tafakari za matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo yote yale wanayohifadhi katika sakafu ya nyoyo zao kama faraja na kitulizo. Kuwazika wafu ni changamoto pevu katika maeneo ambamo kuna kinzani, vita na mipasko ya kijamii inayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo, hofu na wasi wasi, tendo la kuwazika wafu linakua na umuhimu wa pekee kama inavyojionesha hata katika Agano la Kale. Kuna hatari kwamba, leo inaweza kushindikana kabisa kuwazika maskini na waathirika wa vita hali ambayo ni ukweli wa mambo!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu siku ile ya Ijumaa kuu: Bikira Maria, Yohane na baadhi ya wanawake waliokuwa chini ya Msalaba hawakujua nini cha kufanya! Lakini, Yusufu wa Arimathaya aliyekuwa ni mfuasi wa Yesu alimwomba Pilato kuuzika mwili wa Yesu kwenye kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Hili ni tendo la huruma lililotekelezwa kwa ujasiri mkubwa na kwamba, kwa Wakristo kuzika wafu ni tendo ibada na kielelezo cha imani na matumaini katika Fumbo la Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Ibada ya kuwaombea wafu inapewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa hasa wakati huu wa Mwezi Novemba.

Baba Mtakatifu anasema, kuwaombea marehemu ni kutambua ushuhuda walioacha nyuma yao pamoja na mambo mema waliyotenda katika hija ya maisha yao. Ni tendo la kumshukuru Mungu kwa zawadi ya upendo na urafiki wao na kwamba, Kanisa kwa namna ya pekee linasali na kuwaombea Marehemu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwakumbuka wale waliotangulia katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu. Sala hii ina maana ya pekee kwani, inawawezesha waamini kuwaweka mbele ya huruma ya Mungu ndugu na jirani zao, kwa matumaini kwamba, wataweza kuungana na Kristo Yesu kwenye maisha ya uzima wa milele, ili siku moja, wote kwa pamoja waweze kuonja na kushiriki Fumbo la upendo ambalo kwa sasa bado halijafahamika vyema lakini wanauhakika wa uwepo wake kwani hii ni ahadi iliyotolewa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga utamaduni wa kuwaombea wazima wanaoendelea kupambana pamoja nao katika majaribu ya maisha na kama sehemu ya imani ya Kanisa kwa kukiri “umoja wa watakatifu” unaoonesha uzuri wa huruma ya Mungu iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Umoja wa Watakatifu unadhihirisha kwamba, wote wamezamishwa katika maisha ya Mungu na wanaishi katika upendo huo. Wazima na wafu, wote wako kwenye umoja kwani wamepokea zawadi ya Ubatizo, wakalishwa kwa Mwili wa Kristo, yaani Ekaristi Takatifu na kwamba, wanaunda familia kubwa ya Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna njia nyingi za kuwaombea jirani na zote ni sawa na zinakubalika mbele ya Mwenyezi Mungu, ikiwa kama zinatekelezwa kwa moyo wa dhati. Hizi ni sawa na baraka zinazotolewa na wazazi kwa watoto wao; sala kwa wagonjwa hata wakati mwingine kwa ushuhuda wa machozi katika hali tete na ngumu. Lakini pia pale watu wanapopata habari ya furaha! Roho Mtakatifu anawasaidia waamini katika udhaifu wao katika kusali, lakini wanapaswa kufungua nyoyo zao ili kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuzisafisha na kuzitakasa, ili kuziwesha kufikia hatima yake.

Waamini waombe daima kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kama wanavyosali katika Sala kuu ya Baba Yetu! Kwa hakika, Mwenyezi Mungu hatawaacha kamwe anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kwa kuhitimisha tafakari kuhusu matendo ya huruma: kiroho na kimwili, sasa ni wakati wa kusali na kuombeana ili kweli matendo ya huruma: kiroho na kimwili yaweze kuwa ni vinasaba na mtindo wa maisha ya waamini. Kipindi cha Majilio, waamini wanaposubiri ujio na hatimaye, kuweza kukutana na Kristo Yesu anayezaliwa tena katika maisha yao, iwe ni fursa ya kuombeana, ili kuweza kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.