2016-11-30 07:25:00

Amoris laetitia ni kwa ajili ya huduma ya Injili ya familia!


Baba Mtakatifu Francisko kupitia Wosia wake wa Kitume Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya familia, anaonesha kuheshimu na kujali changamoto ambazo familia zote wanakumbana nazo kwa namna moja au nyingine. Kardinali Lorenzo Baldisseri, katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu amesema kuwa, Wosia huo wa kitume umefika kwa wakati muafaka ambapo familia zimo kwenye kinzani kubwa kihistoria. Kinzani kutambua wajihi wake, kujitambua kijinsia mwanamke na mwanaume, kuheshimu tunu ya ndoa na familia, kutunza uhai na haki msingi za watoto na kila mwana familia, kujaliana na kupendana kwa furaha.

Wosia wa kitume, Amoris laetitia, unaeleza kwamba ni ngumu kuwatia moyo wana ndoa kuhusu uaminifu na kujitoa kwa kila mmoja bila kutia cheche hija ya kukua, kukomaa na kuzama katika upendo kati ya wana ndoa na ndani ya wanafamilia wote. Kwa sababu upendo ndio chemichemi na msingi wa ndoa, na upendo huo katika kukua na kukomaa kwake unarutubika na kupanuka kwa kuzaa na kulea watoto, na kuwashirikisha jamii nzima matunda ya upendo kwa mahusiano ya uaminifu na ukarimu kidugu.

Ndoa ni mahusiano ya dhati yaliyosheheni upendo na maisha. Neno upendo ingawa linatumika sana na watu, mara nyingi halifahamiki vizuri au kutumika kwa namna ambayo ni sahihi. Mtume Paulo akilitambua hilo, anaandika utenzi mzuri juu ya upendo: Mwenye upendo huvumilia, hufadhili, mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni. Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira, haweki kumbukumbu ya mabaya, hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli. Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote. (Rej., IWakorintho 13, 4-7). Wosia huo wa kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia, unalenga kuamsha ari na kupyaisha maisha ya ndoa na familia kwa kufuata misingi ya Injili na mafundisho tanzu ya Kanisa mintarafu ndoa na familia. Ni muhimu sasa, kila mmoja ashiriki na kuweka bidii katika kubadilika na kupyaisha kwanza kabisa mtazamo, na pili namna ya kuishi upendo, ndoa na familia.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu ndoa na familia, walikubaliana kwa moyo radhi kwamba katika parokia, ambayo ni familia ya wakristu inayojumuisha familia nyingi, panapatikana mchango mkubwa sana na wa msingi kwa maisha ya ndoa na familia. Kwa sababu hiyo, ni muhimu kudumisha utamaduni wa malezi endelevu ya ndoa na familia, kuanzia vijana wadogo, kwa wachumba, na kwa wana ndoa. Ni lazima kuendelea kuwafundisha na kuwasaidia waamini kuvumbua kila siku utajiri, thamani na uzuri unaopatikana katika maisha ya ndoa na familia. Katika ndoa na familia kuna umoja na mshikamano mkamilifu, unaochangia katika mshikamano wa jamii, na kuyapa maana halisi mahusiano ya jinsia ambayo ni zawadi Mungu anamtunukia mwanadamu. Ithaminiwe pia kuwa, ndoa na maisha ya familia vinachangia sana malezi na makuzi mazuri ya watoto.

Wachungaji makuhani wanapotoa huduma zao kwa wanafamilia, waoneshe ukaribu wa kibaba na kuwasindikiza katika magumu yao, hasa kwa miaka ya awali baada ya kufunga ndoa. Wachungaji makuhani, wazingatie sio tu walio katika ndoa, bali wawajali na kuwasindikiza kwa upendo wa kibaba, wale ambao kwa namna moja au nyingine wamejikuta kwenye hali ambazo maisha ya ndoa yameingia dosari na kuwavuruga, na pengine kupelekea familia kujikuta katika vidonda na maumivu. Wawahudumie kwa namna ambayo watapata faraja, na kuwasindikiza katika hija ya maisha, ili waweze kubaki waaminifu katika mafundisho na maisha ya kikristu.

Maisha ya ndoa na familia ni safari inayoelekea ukomavu. Kama ambavyo Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili alipendekeza: maisha ya ndoa na familia ni kanuni ya ukuaji tarataibu, kwani mwanadamu anafahamu, anatathimini, anathamini na kuishi sheria ya maadili kufuatana na hatua tofauti tofauti za ukuaji wake. Hivyo wachungaji makuhani lazima wazingatie kanuni hiyo ya ukuaji wanapowahudumia wana ndoa, wanafamilia na wale ambao wamejikuta kwenye utengano na maumivu sababu ya matukio kadhaa ya kimahusiano.

Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake amehimiza sana tathimini ya dhamiri na uleaji wa dhamiri safi. Dhamiri ni makao ya siri na mahala patakatifu ambapo mwanadamu anazungumza na Mungu wake katika kweli na uaminifu (Gaudium et seps 16). Iwapo mwanadamu atazingatia usafi na ukweli wa dhamiri yake, makundi mengi yanayoshabikia mambo machafu na yasiyofaa, yataanza kujitenga na ushabiki huo, na pole pole wataweka juhudi za kuishi kanuni safi za maadili.

Kwa mwendo huo wa kujitathimi dhamiri, changamoto nyingi za kimahusiano na familia zitapata ufumbuzi na kurudi kwenye kanuni na mafundisho ya Kanisa kama atakavyo Mungu, mfano suala la utambuzi wa wajihi kijinsia, uaminifu katika ndoa, ndoa moja na halali ndani ya Kanisa, ndoa kati ya mwanamume na mwanamke, ndoa ya mke mmoja na mume mmoja, malezi bora ya watoto, utunzaji na uteteaji wa zawadi ya uhai, heshima ya utu wa mwanadamu, kuzingatiwa haki msingi za binadamu, biashara na uwekezaji halali katika kujipatia kipato kifamilia, ukarimu na kusaidia wahitaji, familia kuwa mfano bora wa maisha kwa jamii inayowazunguka, ushirikishwaji wa heshima kwa wanawake katika masuala mengi ya kijamii kadiri ya uwezo na maumbile yao, kuheshimu na kutunza mazingira Nyumba ya wote.

Kwa sababu hiyo, kila mwamini adumishe ule utamaduni wa kufanya tathimini ya kina ya dhamiri kila siku: kujitathimini matendo ya kila siku iwapo ameyatenda kufuatana na mapenzi ya Mungu, iwapo amekuwa mkarimu, mwenye kujali na mwaminifu kwa kila mtu na kwa Mwenyezi Mungu, ajitathimini iwapo aliyowatendea wengine angefurahia kutendewa mwenyewe, sababu Bwana asema: yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndio maana ya sheria ya Musa na mafundisho ya manabii.  (Rej., Mathayo 7: 12). Mwanadamu ajitathimini kutoka katika undani mwa dhamiri yake, mahali anapozungumza na Muumba wake, na ayachanganue kwa uaminifu na katika kweli, matendo yake mbele ya Mungu, hata kama wengine hawayafahamu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.