2016-11-29 08:44:00

Wimbi kubwa la wahamiaji na ukosefu wa ajira ni changamoto pevu Ulaya!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 28 Novemba 2016 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Ireland, “Taoiseach”, Enda Kenny ambaye baadaye alipata nafasi ya kukutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallegher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa katika mazungumzo yao wamegusia mahusiano mazuri yaliyoko kati ya Vatican na Ireland pamoja na mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Ireland hususan katika sekta ya elimu. Wamejadili pia umuhimu na ushiriki wa Wakristo katika maisha ya hadhara, hasa katika mchakato wa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kuanzia kwa wanyonge na wasioweza kujitetea wenyewe.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wameendelea kujielekeza zaidi katika masuala ya Bara la Ulaya, kwa kugusia kwa namna ya pekee wimbi kubwa la wahamiaji, ukosefu wa fursa za ajira hasa kwa vijana wa kizazi kipya; changamoto kubwa kwa Bara la Ulaya kwa wakati huu, mwaliko kwa Serikali na taasisi kushughulikia changamoto hizi kwa kisiasa na kitaasisi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.