2016-11-29 13:39:00

Fadhila ya unyenyekevu itawaletea hekima ya kimungu


Mwenyezi Mungu huwafunulia wadogo na wanyonge mafumbo makuu ya imani na ndio huwatumia katika mpango wake wa wokovu. Wakati wa mahubiri siku ya Jumanne, tarehe 29 Novemba 2016, kwenye Kikanisa cha Mt. Martha, mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini kuwa wanyenyekevu ili kupata kufunuliwa mafumbo ya imani na kushirikishwa katika kazi ya Mungu ya kumkomboa mwanadamu. Kipindi cha Noeli ukuu huo wa Mungu kuwainua na kuwatumia wadogo huonekana katika mifano ya watumishi wake wanyenyekevu. Watu wenye unyenyekevu wanaojaliwa kufahamu na kutenda makuu ya Mungu.

Bikira Maria binti anayepewa dhamana ya kumbeba na kumlea mtoto Yesu, na katika unyenyekevu anayapokea yote na kuyatenda kwa uaminifu mpaka mwisho. Kukutana kwa Bikira Maria na Elisabeth, ni mifano ya wajakazi wawili wenye utulivu, moyo wa ukarimu na kujali. Yohane Mbatizaji ambaye anamtambua Bwana tangu wakiwa tumboni, na hivyo anaruka kwa furaha. Mtakatifu Yosefu, anayekuwa baba mlishi wa Yesu, anapokea maagizo ya Mungu katika njonzi na anabaki kuwa mwaminifu kuitunza familia hiyo takatifu.

Wapo wachungaji kondeni ambao malaika anawapelekea ujumbe wa furaha wa kuzaliwa Bwana, habari inayotangazwa kwao wanyonge na sio katika majumba ya wafalme. Kuna mamajusi ambao kupitia sayansi ya utabiri wa nyota,  wanafunuliwa juu ya kuzaliwa kwa mtoto Yesu. Pia kuna watoto ambao wanauwawa kwa amri ya Herode, katika unyonge wao wanakufa mashahidi sababu ya mtoto Yesu na kushiriki katika kazi ya Mungu kumkomboa mwanadamu.

Katika unyenyekevu mbele ya Mungu, waamini wanapata ulinzi na kutiwa nguvu na Mungu mwenyewe, kiasi cha kuwawezesha kutenda mambo makuu na kuwastaajabisha wengine. Unyenyekevu huo lazima uchote hekima kutoka kwenye uchaji wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujifunza unyenyekevu na kudumu katika uchaji wa Mungu, wala sio woga. Kwa namna hii watadumu kwenye hija ya maisha kwa furaha na matumaini.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.