2016-11-28 07:54:00

Mpokeeni Mungu na jengeni ufalme wake wa haki na amani duniani!


Mwaka mpya wa Kanisa unaofunguliwa rasmi kwa Kipindi cha Majilio ni safari mpya ya imani ya watu wa Mungu inayowakumbusha kwa namna ya pekee, Ujio wa kwanza wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu katika Fumbo la Umwilisho, pale Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kuzaliwa na Bikira Maria kwenye Pango la kulishia wanyama mjini Bethlehemu. Mwenyezi Mungu anaendelea kila siku kuwatembelea na kuandamana na watu wake bega kwa bega katika hija ya maisha yao. Ujio wa tatu ni pale Mwenyezi Mungu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho, kama Kanisa linavyokiri kwenye Kanuni ya Imani. Injili ya Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio, imejikita katika tafakari ya mambo ya nyakati!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 27 Novemba 2016 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa macho, makini na kukesha na kamwe wasiishi kwa mazoea kwani hawajui siku wala saa atakapokuja Mwana wa mtu kuwahukumu wazima na wafu! Kuhusu gharika na madhara yake, Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili haitaki kuwaogopesha watu na majanga asilia, bali kuwasaidia kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha kwa kutumia rasilimali ya dunia kwa ukomavu na busara pamoja na kufanya maamuzi makini katika maisha.

Waamini wajenge na kuimarisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu anayekuja kuwatembelea na kuambatana nao katika safari ya maisha yao hapa duniani, mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha ili kila jambo wanalofikiri na kutenda, liweze kuwa na thamani mbele ya Mwenyezi Mungu anayewatembelea. Huu ni mwaliko wa kuwa na kiasi anasema Baba Mtakatifu Francisko, ili kutomezwa sana na malimwengu, bali kuutawala ulimwengu na vyote vilivyomo, ili kutambua mambo msingi katika maisha, yaani kuwa tayari kukutana na Mwenyezi Mungu anayekuja kuwatembelea. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha “falsafa ya samaki” yaani kukesha daima, kwani hawajui siku wala saa atakapokuja Mwana wa mtu!

Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka kwa waamini kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika nyoyo zao, ili kutomezwa na malimwengu yanayoendelea kupyaishwa kila kukicha; kwa kutojiamini na kujitegemea katika miundo mbinu, ngome na usalama binafsi kwani Mwenyezi Mungu atakuja siku na saa wasioyodhani hata kidogo, ili kuwashirikisha mwelekeo mpya na mpana na ulio mzuri zaidi. Bikira Maria, Mama wa majilio awasaidie waamini kutambua kwamba, wao si wamiliki wa maisha yao hapa duniani, wawe tayari kumruhusu Mungu anapowatembelea ili kuwaletea mabadiliko ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.