2016-11-28 08:39:00

Familia ya Mungu Mbulu, endeleeni kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa makini kwa familia ya Mungu kurejea tena na tena katika Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya katekesi ya kina kuhusu huruma na upendo wa Mungu kiini cha mafundisho makuu ya Kanisa. Imekuwa ni nafasi ya kutafakari matendo ya huruma kiroho na kimwili, tayari kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu kama kielelezo cha imani tendaji, upendo na mshikamano unaogusa mahangaiko ya jirani, tayari kuyapatia jibu makini linalofumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, imekuwa ni nafasi ya kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika Mafumbo ya maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa katika Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Kimekuwa ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; majadiliano ya kidini na kiekumene, changamoto kwa sasa ni kuendelea kushuhudia matunda yaliyovunwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kama yalivyokuwa yamebainishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Waraka wake wa kitume, Uso wa huruma “Misericordia vultus”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Lango la huruma ya Mungu, yaani Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, ukabaki wazi, huo ni mto wa rehema unaobubujisha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wakimbilie huruma hii anasema Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kitume, Huruma na amani; “Misericordia et misera”, katika maisha na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na msamaha! Kwa njia ya kusikiliza, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma na mapendo. Ni wakati wa kukimbilia huruma, upendo na msamaha wa dhambi katika sacramenti ya Upatanisho, ili kuonja faraja na uponyaji wa ndani.

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuwajali, kuwahudumia na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kimsingi, huu ndio mwendelezo makini wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki Moshi ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Mbulu, wakati wa kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Jimbo Katoliki Mbulu, ameitaka familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mbulu, kuendelea kujikita katika umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo kwa jirani zao; kwa kupokea na kutoa msamaha kwani wanahamasishwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni!

Askofu Amani amewakumbusha waamini kwamba, kila mara wanapotenda dhambi wanajitenga na upendo wa Mungu, kumbe, waendelee kujibidisha kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kutotenda dhambi, lakini pale wanapoelemewa na dhambi pamoja na udhaifu wa kibinadamu, basi wasisite kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu anasema Askofu Amani. Kumbe, toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma ni mambo ambayo yanapaswa kuendelea kupamba maisha ya waamini hapa duniani, hadi pale watakapoungana na Baba mwenyehuruma mbinguni kwa ajili ya kufurahia maisha ya uzima wa milele! Ikumbukwe kwamba, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili, yaliyoongezwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni.

Hivyo, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani uchafuzi wa mazingira una madhara makubwa kwa maisha, utu na heshima ya binadamu! Athari za mabadiliko ya tabianchi ni janga ambalo kwa kiasi kikubwa ni matunda ya kazi ya mikono ya binadamu, lakini, wanaoteseka zaidi ni maskini! Askofu Isack Amani kwa kuonesha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira na ekolojia ya binadamu, alishiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti ya kivuli na matunda katika eneo la Parokia ya Sanu, Jimbo Katoliki Mbulu, kielelezo cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Sr. Edith Temu na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.