2016-11-28 14:02:00

Dunia inahitaji wanasayansi wasiotafuta masilahi binafsi


Katika mkutano mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ulioanza mjini Vatican, mwishoni mwa juma (25 – 29 Novemba 2016), Baba Mtakatifu Francisko kawashukuru na kuwapongeza wadau wote kwa mchango wanaotoa kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwenye mahusiano kati ya wanadamu, na kwa namna ya pekee kwenye kujali utunzaji wa sayari dunia, ambamo Mwenyezi Mungu kamuweka mwanadamu ili kuishi.

Hakika kwa nyakati hizi, hitaji kubwa la huduma ya sayansi kwenye changamoto za mabadiliko ya tabia nchi linaonekana, ambapo athari zake zinahatarisha hali za maisha na jamii ya mwanadamu. Juhudi za Taasisi ya Kipapa ya Sayansi zinaleta mwamko sana hasa kwa kuona namna taasisi hiyo inavyojikita katika kutetea haki, amani, utu, uhuru na maendeleo ya binadamu.

Baba Mtakatifu kawakumbusha washiriki wa mkutano huo kuwa, Mungu kampatia mwanadamu mamlaka shirikishi ili kuutunza ulimwengu, mwanadamu akiwa chombo cha Mungu (Rej., Laudato sì, 53). Inasikitisha kuona jinsi mwanadamu anavyotumia ulimwengu na vilivyomo bila kujali nguvu asilia zilizomo kwenye mfumo wa ulimwengu, na bila kujali lengo la maendeleo ya viumbe hivyo kadiri ya mapenzi ya Mungu. Matokeo yake ni kuharibu uzuri na mahitaji yaliyomo, kiasi kwamba badala ya kumfaa mwanadamu, vimeanza kuwa ni hatarishi kwa uhai na usalama wa mwanadamu mwenyewe. Ni wakati wa kurudi kwenye utaratibu alioupanga Muumba, kila mmoja kuwajibika ili kuepuka hatari zinazotokana na matumizi holela ya viumbe yasiyojali utunzaji wa dunia na usalama wa mwanadamu.

Wanahitajika wanasayansi wanaofanya utafiti na kutenda huduma zao bila kufungamana na upande wowote wa masilahi ya kisiasa, uchumi na nadharia. Kuna hitaji la kujenga utamaduni wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika jamii. Dunia na vilivyomo sio faida kwa wachache tu, ni kwa ajili ya manufaa ya wote.

Jumuiya za wanasayansi zinapaswa kutafuta suluhu za kukabiliana na changamoto za nishati ya maji, nishati zingine na lishe. Lazima kuwe na kanuni madhubuti na ziheshimiwe na wanasayansi wote ili kuhakikisha ulinzi na utunzaji thabiti wa viumbe hai. Hii itakuwa namna nzuri na salama ya kuepuka madhara kwa mazingira, kwa jamii, demokrasia, haki na uhuru. Jumuiya ya kimataifa na sera zake imeonekana kuwa dhaifu sana katika kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabia nchi na athari zake, amesema Baba Mtakatifu Francisko, lakini wasisahau dhamana wanayopewa na Mungu na raia ili kulinda na kutetea mafao ya wote, na sio manufaa kwa wachache.

Pamoja na kutotiliwa mkazo wa kutosha kwa upande wa jumuiya ya kimataifa, kuna ishara za kutosha za matumaini zinazoonekana kutoka kwa wenye nia njema ya kutafuta mafao ya wengi, kulinda na kutunza vema mazingira anamoishi binadamu na viumbe wengine. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanasayansi kuunganisha nguvu kwa pamoja, huku wakizingatia maadili, ili kuwekeza kwenye maendeleo endelevu na yanayofumbata mahitaji na usalama wa mwanadamu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.