2016-11-26 16:15:00

Papa anawataka vijana kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani!


Imegota miaka kumi na mitano tangu Serikali ya Italia ilipoongeza muda wa vijana nchini Italia kujitolea katika huduma za kijamii kwa kutumia muda wao ziada, kielelezo cha utajrii mkubwa wa jamii pamoja na wale wanaofaidika na huduma hii. Hii ni sehemu ya mchakato wa makuzi endelevu ya binadamu. Vijana ni nguvu na jeuri ya jamii, muhimu sana katika kutekeleza mafao ya jamii kwa lengo la kuendeleza usawa na udugu.

Pale ambapo kunakosekana kwa usawa wa kijamii au kati ya mataifa; pale ambapo huduma kwa wanyonge na maskini hazipewi kipaumbele cha pekee na badala yake jamii inawekeza zaidi kwenye biashara na ununuzi wa silaha au mbaya zaidi maskini na wanyonge wanapoonekana kuwa ni kero, badala ya kusaidiwa, hapo jamii inaogelea katika dimbwi la maji machafu! Hii ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 26 Novemba 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na kundi kubwa la vijana wanaojitolea katika huduma za kijamii nchini Italia.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mielekeo ya namna hii ni kielelezo hasi cha kuumbuka kwa jamii na utamaduni wake kwa kukumbatia vigezo na utekelezaji ambao unawatenga na kuwaelemea watu kiasi cha kuendelea kutumbukia katika umaskini si tu wa maisha kwa wale waliosahaulika au kutengwa na jamii lakini hata na wale wengine wanaoishia kujifunga katika ubinafsi wao, kiasi cha kushindwa kukutana na jirani zao, chachu ya kutafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao wanatekeleza wajibu wao katika mazingira magumu ambayo wakati mwingine yanakwenda kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu. Hii ni huduma  ya kinabii inayoonesha jinsi ambavyo inawezekana kufikiri na kutenda tofauti kabisa na mwelekeo wa jumla. Kati ya huduma makini za kijamii zinazotolewa na vijana hawa, utunzaji bora wa mazingira unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hii ni huduma ya ekolojia ya binadamu!

Hapa watu wanatambua uhusiano wa karibu uliopo kati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; heshima kwa binadamu pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maisha ya watu, lakini zaidi maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”! Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji msaada na kuingizwa katika mafungamano ya kijamii ni muhimu sana na kwamba, Italia imekuwa mstari wa mbele katika huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji inayopaswa pia kuendelezwa na kudumishwa kwa kuonesha ukarimu na ushirikishwaji wa makundi haya ya watu katika jamii.

Huduma ya elimu ni kati ya nyanja zinazofanyiwa kazi nchini Italia, kwa kuwasaidia watoto, walemavu na wale wote wanaohitaji msaada. Kwa wakati huu, Baba Mtakatifu anasema, mawazo na huduma yao imeelekezwa zaidi kwa waathirika wa matetemeko ya ardhi na mafuriko. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia nchini Italia kwa siku za hivi karibuni. Matukio yote haya yanakuwa ni fursa ya ukuaji wa kiutu, mang’amuzi, ufahamu pamoja na kuguswa na mahangaiko ya watu!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kufuata njia ya maisha inayowapatia furaha katika maisha yao, kadiri ya zawadi na karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu na mazingira yao. Huduma kwa watu ni muhimu sana katika jamii na inawawezesha watu wengi zaidi kufarijika na kunufaika na  huduma hizi, changamoto ya kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa huduma za kijamii. Vijana wanahamasishwa kufuata njia hii ya ukamilifu inayoonesha ubinadamu wa Yesu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kiasi cha kumimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa wengi.

Baba Mtakatifu anazishukuru taasisi zinazotoa fursa kwa vijana kwa kipindi cha mwaka mmoja kuweza kutoa huduma za kijamii; anazitaka ziendelee kuonesha ari na moyo wa mshikamano na jamii inayowazunguka ili kudumisha mwingiliano wa kijamii, katika maisha binfasi na yale ya hadhara. Utamaduni wa jamii ya watu unapimwa kutokana na uwezo wake wa kuheshimu na kuendeleza haki msingi za binadamu, hasa miongoni mwa maskini na wanyonge zaidi. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuendelea kuwa na mwelekeo na mtazamo mpana wa huduma na kujisadaka kwa ajili ya wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.