2016-11-26 16:31:00

Kanisa litaendelea kumshukuru Papa Mstaafu Benedikto XVI


Akitoa shukrani na kuwapongeza washiriki wa Kongamano la kimataifa kuhusu mambo ya nyakati, escatologia, Jumamosi, tarehe 26 Novemba 2016 Baba Mtakatifu Francisko ametambua umuhimu na upendo wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, kwenye mafundisho ya Kanisa, ambaye bado anaendelea kuliombea Kanisa na watumishi wake kama alivyoahidi wakati wa kung’atuka kwake, kutoka kwenye Kiti kitakatifu cha Khalifa wa Mtume Petro.

Kongamano hilo lilifanyika katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu, na kuhitimishwa katika Taasisi ya mafundisho ya mababa wa Kanisa, Augustinianum, jijini Roma. Tukio hilo la hitimisho limeenda sambamba na shamrashamra za kutunuku Tuzo ya Joseph Ratzinger – Benedikto XVI. Kwa wahusika waliojitokeza zaidi katika tafakari za kisayansi mintarafu taalimungu kama sehemu ya mwendelezo wa urithi mkubwa ulioachwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, wakati wa uongozi wake kwenye Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa, na baadaye akiwa khalifa wa Mtume Petro, mafundisho juu ya mambo ya nyakati, escatologia, yalichukua nafasi ya muhimu sana. Msisitizo na uchambuzi makini juu ya maisha ya milele na matumaini, yalifafanuliwa vizuri sana katika barua yake ya kitume Spe salvi, yaani Tumaini la wokovu. Habari na mafundisho juu ya mambo ya nyakati ni muhimu sana kwa ajili ya kutafakari maana na lengo la maisha ya mwanadamu, na kuepuka kuridhika na mambo ya dunia, ambayo yatapita, hali mwanadamu anapaswa kuishi milele. Kwa sababu hiyo Mtume Paulo anahimiza waamini akisema: basi ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, sio yaliyo katika nchi. (Rej., Wakolosai 3: 1-2).

Katika hotuba yake kwenye sherehe za kutunuku tuzo ya Joseph Ratzinger, Baba Mtakatifu Francisko, amekumbusha jinsi maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu yalivyokuwa fursa kufafanua jinsi gani matendo ya huruma yatakuwa ndiyo itifaki ya hukumu ya mwisho ya mwanadamu, kadiri ya mafundisho ya Kristu: nalikuwa na njaa mkanipa chakula, nalikuwa na kiu mkanipa kinywaji (Rej., Mathayo 25:35).

Mafundisho ya kina ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI yanachota upeo wake kutoka kwenye chemichemi ya Maandiko Matakatifu na mafundisho ya Mababa wa Kanisa, wakati huo huo yanarutubishwa kwa imani thabiti na sala. Namna hiyo ya tafakari, uchambuzi na ufundishaji imekuwa lishe yenye rutuba sana kwa imani na maisha ya waamini, ikitoa msaada wa kuelewa msingi wa shughuli za kila siku za mwanadamu na tumaini waliloitiwa waamini, kufunguka kuelekea maisha ya milele, ambalo ni lengo la mwisho la mwanadamu.

Mafundisho ya Benedikto XVI yamekuwa rutuba iliyojikita katika misingi thabiti ya maisha ya kikristu, ambayo ni Kristo Bwana na mwokozi aliyefanyika mwili, akateswa, akafa, na kufufuka, ukarimu, matumaini na imani. Kwa hakika, Kanisa zima litajivunia siku zote hazina hiyo ya baba Mtakatifu mstaafu Benedikto  XVI, na halitakoma kumshukuru kwa yote aliyofundisha na kuelekeza. Waliotunukiwa tuzo ya Joseph Ratzinger kwa mwaka 2016 ni Monsinyo Inos Biffi na Jalimu Ioannis Kourempeles. Monsinyo Biffi ametunukiwa tuzo hiyo kwa heshima ya maisha na kazi alizotenda kwa kujikita kwenye mafundisho ya Kanisa kwa muda wote. Jarimu kijana kabisa Ioannis Kourempeles, ametunukiwa tuzo hiyo kwa kutambua mchango wake mkubwa mpaka sasa katika kuchanganua mawazo ya Joseph Ratzinger – Benedikto XVI na mafundisho msingi ya Kanisa la Kiorthodox katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.