2016-11-26 17:13:00

Kaeni mkao wa kula msije mkaisoma namba!


Oyaaaa! Kumekucha, kaeni mkao wa kula! Mambo yameiva! Kila mwaka tunaalikwa kufungua macho kuuangalia ujio wa ulimwengu mpya unaoletwa na Yesu. Fasuli ya Injili leo imepachikwa katika mazingira yaliyomfanya Yesu kusema maneno mazito. Tutajaribu kuyafuatilia maneno hayo katika maisha yetu tupate kujitayarisha vyema kwa ujio wa Bwana. Mazingira hayo yalikuwa hivi: Siku moja wanafunzi walimwalika Yesu kulishangaa hekalu la Yerusalemu jinsi lilivyojengwa vizuri na kwa ustadi wa hali ya juu.

Hekalu kwa Myahudi lilikuwa alama ya kudumu na ya uimara. Myahudi alijisikia salama mbele ya Mungu na hivi kujisikia kuwa dini yao ilikuwa imekamilika. Kadhalika mahusiano na watu yalikuwa safi kwani ilitosha tu kwao kufuata Tora. Kwa hiyo hekalu la Yerusalemu lisingeweza kamwe kuangamizwa. Yesu anapoalikwa kulishangaa hekalu hilo, anatoa bomu linalowashangaza wafuasi wake anaposema: “haya yote mnayoyaona yataangamizwa.” Kwamba ulimwengu wa zamani utaanguka, na badala yake utakuja ulimwengu wenye picha mpya ya Mungu na mahusiano ya watu yatakuwa tofauti kabisa.

Mfano wa hali halisi ya ulimwengu mbovu wa zamani ni ule wa wakati wa Nuhu ambao Mungu aliufifisha kwani hakukubaliana nao. Mbele ya Mungu dunia ilikuwa imeharibika na kuchafuka kwa ukatili, kwa kukandamizana na kwa kunyanyasana. Hili neno ukatili linatajwa karibu mara mbili katika sura ya sita ya kitabu cha mwanzo. Hadi Mungu akaamua kuingilia kati na kuufutilia mbali kwa njia ya gharika na kuleta ufalme mpya. “Ya kale hayako.”

Kwa Kigiriki ujio unaitwa Parousia. Ujio huo ulikuwa wa kiongozi, wa mfalme, wa mtawala, au wa mkuu yeyote aliyetembelea na kukagua sehemu fulani, kuona mazingira na kuyabadili au kuyarekebisha. Watu wengine hawakupenda sana ujio huo, kwani iliwabidi kufanya kazi ya kuandaa pahala atakapopita, kama vile kutengeneza barabara, kubomoa sehemu zisizotakiwa ili kuboresha mazingira. Kwa wengine, ujio huo ulisubiriwa kwa hamu kwani ulikuwa ni motisha ya matumaini mapya waliyokuwa wanayategemea kuyaona kwani, “Mgeni afike mwenyeji apone.” Yesu anatoa mifano mitatu ili kuelewa vyema hali halisi inayoweza kutokea  wakati wa ujio wa mabadiliko hayo.

Mfano wa kwanza: “Kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina.” Mfano huu unavielekea vikundi viwili vya watu: Kikundi cha kwanza ni cha watu wa maisha ya kawaida ya kula, ya kunywa na kuoana. Tunadokezewa kwamba, watu hawa hawakuwa wabaya, bali wao walijikita kwenye kula, kunywa, na kuoana. Kasoro yao ni kwamba hawakuelewa kama kungetokea mabadiliko. Hawakufunguka macho kuuona ulimwengu mpya, badala yake wao waliishi maisha ya kibaolojia tu ya kula na kunywa na kuoana mwisho. Aidha, hapa tunaletewa picha ya gharika na ieleweke hivyo kuwa ni picha tu siyo jambo la kihistoria. Ingeweza hata kuwa picha ya moto unaounguza. Onyo ni kwa watu kutobweteka kama kibatari na hatimaye, wakakiona kilicho mnyoa Kanga manyoya!

Kumbe, picha hii ya gharika imechukuliwa kutoka mandhari ya nchi tambarare ya Mesopotamia iliyokuwa kati ya mito miwili mikubwa Tigris na Eufrates. Mito hii ikifurika ilikuwa inaleta uharibifu mkubwa sana. Lengo ni kuonesha kuwa Mungu hapendi ulimwengu ule wa kale. Kwa hiyo gharika ni hukumu ya Mungu juu ya maisha ya kila mtu. Siyo kwamba Mungu anakuja kukuharibu, la hasha bali anakutahadharisha kwamba kama hupokei ujumbe mpya utokao mbinguni, maisha yako yanapoteza thamani na yatakuwa si kitu, nawe utakuwa nje ya historia ya Mungu. Ni muhimu kufaidi maisha ya ulimwengu huu, lakini maisha ya utu na ubinadamu siyo mwisho hapa tu. Mungu hakuwaangamiza kweli watu hawa, bali ni picha inayotolewa kuonesha kwamba msirudie tena makosa yanayooneshwa hapa katika kitabu cha mwanzo.

Kikundi cha pili, ni kile cha familia moja iliyookoka: “hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina.” Familia hii iliokoka kwa sababu ilijali na kutambua kwamba ulimwengu wa kale unaisha na ulimwengu mpya unatokea. Kwa kawaida familia kama hizo ni chache sana. Kwa sababu binadamu tunaishi bila kufikiri na tunakosa kufunguka macho kwa matukio ya mambo. Tunaishi bila kufikiri juu ya maisha yanavyotokea bali tunafuata maisha ya kibaolojia tu. Hapa ni sawa na bendera kufuata upepo tu!

Mfano wa pili: Unawaelekea makundi mawili ya watu wenye shughuli tofauti. Kundi la kwanza ni la wafanyakazi wenye shughuli za pekee au kazi za kitaalamu: “watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atatwaliwa, na mmoja ataachwa.” Watu hao wako katika hatari ya kuzifanya kazi zao kuwa kipeo cha maisha, ni kama mungu wao na kikomo cha maisha yao. Mapato yake wanajikitika moja kwa moja katika kazi. Kumbe kuwajibika huko kunatakiwa kuwe kwa ajili ya ulimwengu mpya. Mapato yake mmoja anatwaliwa na mwingine anaachwa.

Neno hili kutwaliwa limefasiriwa vibaya sana kutoka neno la Kigiriki paralambanetai, tafsiri ya kiingereza ni “being taken along” maana yake kujizatiti au kujikita, kujiingiza kidhati katika kufanya kazi kadiri ya mapendekezo ya habari njema ya upendo, yaani mtu anayefikiria wengine na kutumia utaalamu na ujuzi wake kwa ajili ya wengine. Hapa ni mtu kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zake kwa kutumia akili, ujuzi na weledi wake kikamilifu. Mwingine aphietai yaani ataachwa nyuma au tungesema “itakula kwake,””ataisoma namba” kwa vile yeye anaona kazi ni kipeo bila kumfikiria Mungu. Mtu huyo ataachwa hapohapo aphietai. Mathalani, mmiliki wa kiwanda, mwenye fikra za ulimwengu wa kale, atashughulika zaidi katika kujilimbikizia fedha, mali na utajiri, kufanikiwa katika shughuli bila kufikiria wengine.

Kundi la pili ni la wanawake: “Wanawake wawili watakuwa wanasaga, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” Kwa kawaida wanawake walikuwa wanasaga unga wa ngano na kutengeneza mikate yaani chakula cha maisha. Kila mmoja anatakiwa aandae chakula kwa ajili ya ndugu. Kwa hiyo shughuli hii ya kuandaa chakula cha maisha, chakula hicho si lazima kiwe cha tumbo peke yake, bali chaweza kuwa chakula cha kiakili kinachoweza kutufanya kuwa na utu, chakula cha upendo kinachoweza kumfurahisha mwingine. Mtu huyo atakuwa amepokea na kujikita na ulimwengu mpya. Kumbe mwingine ataachwa katika ulimwengu wa kale wa ubinafsi.

Mfano wa tatu: “kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.” Unatuelekea sisi sote kujilinda daima kwani mwizi anaweza kufika wakati wowote ule usiotegemea na kukuibia. Hapa yaonekana kama vile Mungu ni mwizi anatuibia mali zetu. Ukweli wa mambo mali yote ni ya Mungu, isipokuwa sisi ndiyo wevi tuliojimilikisha mali ya Mungu. Tunajidhani kwamba  kazi zote ni zetu, utalamu tuliona nao ni wetu na maisha yote unayofaidi ni mali yetu. Hivi tunaona kama vile tunaibiwa na tunafirisiwa na kunyang’anywa na mwizi. Kumbe, Mungu siyo mwizi bali ni wewe hukuviona vitu hivyo kwa mtazamo utakiwao.

Kwa hiyo Yesu anasema, kesheni, kaeni mkao wa mapokezi ya Masiha. Katika kila kazi tunayofanya, tuangalie tunaishije mahusiano yetu na hali halisi ya ulimwengu huu kwani wakati msiodhani Mwana wa mtu hufika, si ujio wa mwisho wa dunia, bali sasa. Mpokee ujumbe mpya unaokujia.

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.