2016-11-25 14:40:00

Ulinzi na usalama ni muhimu kwa maendeleo ya wengi!


Vatican inaendelea kusisitiza juu ya umuhimu usiokwepeka wa Shirikisho la kimataifa la Usalama na Maendeleo, katika kuchangia ulinzi wa mataifa madogo. Katika kikao cha tatu cha Shirikisho la kimataifa la usalama na maendeleo, tarehe 10 November 2016, ndivyo anavyotinga kwa kishindo Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Shirikisho hilo, lenye ofisi zake mjini Vienna, Austria.

Mfano mzuri wa umuhimu huo ni uchapishwaji wa mapendekezo ya Bolzan/Bozen ya mwaka 2008, yanayolenga ushirikishwaji wa mataifa madogo katika mahusiano ya kimataifa. Katika ugawaji wa vifaa tendaji kwa mataifa haya madogo madogo, Shirikisho la kimataifa la usalama na mendeleo liendelee kutoa mwongozo wa jitihada za pamoja kulinda na kutetea haki za watu, wanaoishi katika mataifa hayo madogo madogo, kuzuia kinzani na machafuko, na kutunza mahusiano mazuri katika ngazi zote za serikali na mataifa yaliyo madogo.

Katika kulinda haki na uhuru wa mataifa madogo, na kuchangia mahusiano thabiti na ya wazi kati ya taifa na walio wachache, ni muhimu kutilia mkazo nguvu ya dola, na hasa katika ngazi za chini. Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza juu ya nguvu ya dola kwamba: utume msingi wa nguvu ya dola, ni kuhakikisha mazingira salama, kiasi kwamba kila raia aweze kuishi kwa amani na utulivu. Askari waandaliwe kujitambua kuwa nao ni vyombo vya upatanisho, wajengaji madaraja kati ya watu, na wapandaji amani, na kwamba wameitwa sio tu kuzuia ghasia, bali zaidi kushiriki katika kusimika utaratibu na utulivu uliojengeka katika kweli, haki, upendo na uhuru.

Baba Mtakatifu Francisko hachoki kualika dunia nzima kujenga madaraja kati ya watu badala ya kujenga ukuta, kukuza utamaduni wa mazungumzano badala ya utamaduni wa kukosa uaminifu, hasira na chuki. Mwanadamu akichapa mwendo wa aina hii, anaweza kabisa kushinda uadui na kutojali, kuwa na mapatano, mazungumzano na kusimika familia moja ya udugu na mshikamano. Monsinyo Janusz Urbanczyk anaalika Shirikisho la kimataifa la usalama na maendeleo, kuongeza juhudi za kuleta utamaduni wa kukutana, ili kubomoa kuta zinazogawanya watu. Amehimiza kwamba, ni muhimu katika utendaji wa Shirkisho hilo, wawahusishe mataifa hayo madogo, ili wawe sehemu ya harakati hizo, kwani kitendo hicho tu tayari kitakuwa ni moja ya ujengaji madaraja kati ya mataifa, jumuiya, watu, lugha, dini na tamaduni mbali mbali.

Kuna changamoto kupata mafanikio ya usalama na maendeleo kwa mataifa haya madogo, iwapo hawana wawakilishi katika Shirikisho hilo katika mipango na maamuzi ya kisiasa na maendeleo yanayowahusu. Katika ushirikishwaji huo, wanawake wapewe kipaumbele, kwani wanao uwezo wa kuweka mchango wao wa muhimu kwenye mataifa yao madogo na jamii kwa ujumla, amehimiza Monsinyo Janusz Urbanczyk. Itiliwe maanani pia uwezo wa elimu katika kuchangia ujengaji wa madaraja kwa mataifa madogo. Elimu inachangia sana kwenye upatikanaji wa mani, uvumilivu na kuondoa matabaka na ubaguzi. Mikakati ya elimu hiyo ipangwe kwa kuzingatia pia tunu msingi za maisha, mfano heshima kwa utu wa kila mwanadamu, mshikamano, heshima kwa dini na imani ya wengine. Mwishoni, Monsinyo Janusz Urbanczyk, kawaalika Shirikisho la kimataifa la usalama na maendeleo, kuzingatia maisha ya kiroho na maadili ya mataifa hayo madogo katika kulinda usalama wao na kutafuta maendeleo yao, kwani maisha ya kiroho na maadili ni sehemu ya utajiri wa maisha yao.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.   








All the contents on this site are copyrighted ©.