2016-11-25 08:21:00

Kuwepo kati ya watu kwa ajili ya watu na maendeleo yao!


Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaweka mahusiano ya wanadamu katika mwanga wa Injili, sheria asilia, utu, heshima na mafao ya wengi. Mafundisho Jamii yana kiungo chake msingi kinachofumbatwa katika amani ya wokovu uliokamilika; matumaini yaliyosheheni haki na upendo unaowafanya wanadamu wote wawe kama ndugu wa kweli katika Kristo Yesu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limekuwa mstari wa mbele katika kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika maisha na utume wake.

Kwa mwaka huu 2016, maadhimisho haya yaliyoanza kutimua vumbi huko Verona, kuanzia tarehe 24 - 27 Novemba, 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Kati ya watu”. Binadamu ameumbwa ili kuishi kati pamoja na watu wengine ili kushirikiana nao katika hali zao za maisha. Utengano ni udhaifu unaojenga hali ya kutoaminiana na matokeo yake ni watu kujifungia katika ubinafsi wao. Jamii inapowasaidia watu kama wagonjwa, wazee, wakimbizi na wahamiaji; maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii inakuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu unaowaletea watu faraja katika maisha.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa video uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Novemba 2016 kwa washiriki wa Tamasha la Sita la Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayongozwa na kauli mbiu “kati ya watu”, changamoto na mwaliko kwa watu kujenga utamaduni wa kukutana na wengine, ili kushirikishana: uzoefu, mang’amuzi ya maisha; kupokea na kutoa utajiri wa maisha ya ndani kama njia ya kutajirishana kwa tunu msingi za kiutu, kielelezo makini cha mshikamano na msaada kwa watu wanaoishi katika familia na jumuiya za waamini.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu katika jamii wanaoishi katika hali na mazingira magumu kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, mateso, kazi ngumu pamoja na majaribu ya maisha. Kwa kukutana na kuzungumza na makundi kama haya mtu anaweza kung’amua jinsi ya kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kutambua kwamba, wema una nguvu zaidi kuliko ubaya. Uwepo wa waamini kati ya watu ni ushuhuda wa upendo na faraja; amani na utulivu wa ndani, hasa pale watu wanapoguswa na kutikiswa na matukio makubwa ya maisha kama vile magonjwa na kifo! Yote haya ni sehemu ya fumbo la maisha ya mwanadamu, lakini kwa uwepo kati ya watu, jamii inagundua tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, kuwa kati ya watu ni kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha yao, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mafao ya wengi. Kwa kukaa pamoja, watu wanakuwa na mwelekeo mpana zaidi wa kuangalia mambo pamoja na kushirikishana kazi mbali mbali kama sehemu ya ujenzi wa jamii inayojikita katika umoja na mshikamano bila kuwatenga au kuwakuza watu. Hapa kuna haja ya kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Lakini pale maamuzi msingi ndani ya jamii yanapofanywa na watu wachache amani na mafungamano ya kijamii yako hatarini na matokeo yake anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kuongezeka kwa umaskini, kuyumba kwa amani; utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani kwa sababu ya fedha ndiyo inayotumika kuwa ni kipimo cha ufanisi. Kuwa kati ya watu kunasaidia kuimarisha maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake. Kuwepo kati ya watu ni kushirikishana utajiri wa rangi, tamaduni, kabila na dini, kiasi cha kuwawezesha watu kugusa utajiri unaofumbatwa katika utofauti. Hapa mtu anagusa utu, moyo na uhalisia wa maisha ya watu. Ili kuweza kutatua matatizo na changamoto zinazowaandama binadamu kuna haja ya kuwa na ujasiri kwa kuwasikiliza wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwasaidia kwa hali na mali.

Bikira Maria, mtumishi mnyenyekevu na mwingi wa huruma anaendelea kufanya hija na waamini kwa uwepo wake wa daima, mfano na kielelezo makini cha kuwa kati pamoja na watu bila kumtenga awaye yote! Haya ndiyo matashi mema ambayo Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wajumbe wote wanaoshiriki kwenye Tamasha la Mafundisho Jamii ya Kanisa huko Verona, Kaskazini mwa Italia. Anawashukuru na kuwapongeza wote wanaojibidisha kufundisha na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kama ilivyo kwa Padre Adriano Vincenzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.