2016-11-25 14:24:00

Kituo cha Sakramenti ya Upatanisho chaanzishwa Jimbo kuu Dar es Salaam


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake  wa kitume “Misericordia et misera” anawaalika waamini kuendelea kushuhudia na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa, hasa Liturujia na Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu, Matendo ya huruma kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa ni Sakramenti za huruma ya Mungu. Ni mahali pa kuonja upendo, toba, wongofu wa ndani na msamaha kwani huruma yake ni kuu na huvuka kila vikwazo na vizingiti katika maisha ya mwanadamu! Kwa njia ya huruma, waamini wataweza kumwilisha upendo katika maisha yao!

Familia ya Mungu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jumapili terehe 13 Novemba 2013 iliungana na wanakanisa wote ulimwenguni katika kuufunga rasmi Mlango wa Huruma ya Mungu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu katika ngazi ya majimbo. Adhimisho hilo lilifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akishirikiana na umati wa makuhani wanahudumu katika jimbo hilo pamoja na maelfu ya waamini.

Katika adhimisho hilo Kardinali Pengo aliwaambia waamini wa Jimbo hilo kwamba kufungwa kwa mlango wa Jubilei ya Huruma ya Mungu hakumaanishi kwamba, ni kukoma kwa huruma hiyo katika jamii ya wanadamu. Huruma hiyo imekuwa wazi na imemiminwa katikati yetu tangu kale na itaendelea kumiminwa daima hadi ukamilifu wa dahari. Kwa kulithibitisha hilo Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, katika moja ya maazimio iliyojiwekea kwa mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ni kuanzisha kituo cha Sakramenti ya Upatanisho kwa daima, kituo ambacho kimewekwa katika viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, ambacho kilibarikiwa rasmi na Mwadhama Kardinali Pengo mara baada ya kuhitimishwa kwa ibada ya Misa Takatifu.

Kituo hicho kitaanza kutoa huduma yake kuanzia Jumatatu katika Juma la kwanza la Majilio kwa mwaka Mpya wa kiliturujia wa Kanisa na kitakuwa wazi siku zote za juma isipokuwa siku za dominika tu. Kituo hicho kitakuwa kinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni. Kituo hicho ni wazi kwa waamini wote Wakatoliki kutoka Jimbo Kuu la Dar Es Salaam na hata wageni ambao watalitembelea Jiji hilo la kibiasha na lililo kubwa kuliko yote nchini Tanzania kuijongea Sakramenti hiyo ishara ya uwepo endelevu wa huruma ya Mungu kwa binadamu kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani.

Pamoja na kituo hicho cha Sakramenti ya Upatanisho, Jimbo Kuu la Dar Es Salaam limejiwekea maazimio mengine katika kuufanya Mwaka huo wa Jubilei ya Huruma ya Mungu upate chachu ya kudumu. Maazimo hayo ni pamoja na uwepo wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi kiparokia, siku za maungamo kidekania wakati wa kipindi cha Kwaresma, siku ya kumwombea Askofu mkuu wa Jimbo, Hija katika Kituo cha Hija wakati wa maadhimisho ya sherehe ya kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu ambapo pia kutakuwa na fursa ya kuiona na kusali mbele ya nakala halisi ya Sanda ya Yesu, kufanya matendo ya huruma kidekania na kuwa na siku ya wafungwa kijimbo.

Imeandaliwa na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.