2016-11-25 09:24:00

Dumuni katika mahusiano na Mwenyezi Mungu!


Mzaburi anaanza kwa kusema “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimekutumaini wewe, nisiaibike, adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja”. Haya ni maneno ya Zaburi ambayo Mama Kanisa pamoja na watoto wake huyakariri kila mwanzo wa Mwaka mpya wa Kiliturujia wa Kanisa, maneno ambayo yanaupatia mwanzo huu wa mwaka wa kilitutujia ladha ya upya wa maisha ya mwanadamu ambaye anamgeukia Mungu na kumfanya kuwa tegemeo lake katika maisha ya kila siku. Huu ndiyo utume wa Kanisa kila mara, utume ambao hunuia kumfanya mwanadamu kuiinua nafsi yake, kujielekeza kwake na kupatia Mwenyezi Mungu nafasi ya juu. Ni ujumbe ambao unaonesha maana ya upya huu tunaouanza kwa kuutarajia ujio wa Mungu na pia kutudhihirishia kwamba kila mara tunapojikabidhi kwake tutashinda na hatutoaibika, tunahakikishiwa uwepo wa daima wa upya wa mahusiano yetu na Mungu wetu.

Tunapokianza kipindi hiki kipya cha liturujia katika majira ya Majilio, Mama Kanisa hututafakarisha juu ya ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo: umuhimu wake na namna ambavyo tunapaswa kujiandaa na ujio huu. Kutokana na ukweli kwamba hakuna anayejua wakati huo utakuwa lini jambo la muhimu ni kuwa daima katika mahusiano na Mungu ambaye kama tulivyo mwelezea hapo juu ni tumaini letu, nguzo yetu na pindi tunapokuwa naye hatutoshindwa wala kuaibika. Mantiki hiyo inatuonesha sababu za Mama Kanisa kupyaisha daima kipindi cha liturujia kama ishara ya upyaishaji wa daima wa mahusiano yetu na Mungu na kwa namna hiyo kujiweka tayari “kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.

Somo la kwanza la Dominika hii linaidokeza siku hiyo. Kwanza ni kutukuka kwa Bwana Mungu na nyumba yake yote na hivyo kuwavutia wote kwake: “Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sayuni itatoka sheria, neno la Bwana katika Yerusalemu”. Huu ni ukamilifu ambao umenuiwa na Mungu kukalimishwa katika Kristo, yaani hapa ndipo safari ya ukombozi wa ulimwengu huu ambayo ni utimilifu wa fumbo zima la wokovu inaponuia kuelekea. Lakini tunapoiangalia safari hii, kwa jinsi ilivyoanza na makusudio yako tunagundua kwamba ukamilifu huu si kitu chochote kipya katika mpango wa Mungu bali kuturejesha tena upya katika fumbo la uumbaji wakati vyote vilivyoumbwa na kuwekwa katika ukamilifu: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama ni chema sana”(Mw 1:31). Hivyo tunauona mwisho huu ukiturudisha katika wazo tuliloanza nalo ya upyaishaji wa ulimwengu huu, yaani kuufanya kurudi mwanzo wa uumbaji.

Haiba ya jamii ya mwanadamu katika ulimwengu huo mpya inajifunua katika paji la amani: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu”. Kwa maneno mengine ni kwamba, kitendo cha mwanadamu kumrudisha tena Mungu katika maisha yake na kumfanya awe yote katika yote kinamfanya mwanadamu kuunganika na wengine na kuwa katika hali ya uelewano, upendo, mshikamano na ushirikiano. Dhambi ambayo matokeo yake ni kumwondoa Mungu mioyoni mwetu hutufanya tuwe vipofu, kujitenga na wenzetu na kubaki kujifungia ndani mwetu. Hututengeneza kuwa watumwa wa tamaa zetu na kujenga kuta za kutuzunguka. Hivyo tunajijengea uadui na wengine kwa kuwaogopa, kutokuwaamini hata kuwajali. Tunajawa na kiburi na kudharau wengine. Matokeo ya haya yote ni mfarakano kati ya jamii ya mwanadamu.

Wimbo wa Zaburi unatupatia mwaliko wa kuujongea mwisho huo kwa furaha: “Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana ... kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu niseme sasa, Amani ikae nawe”. Hivyo ni mwaliko wa upyaishaji huu wa maisha yetu, mwaliko wa kufanya juhudi ya kumfanya Mungu awe ndani ya nafsi ya kila mmoja ili sote kujawa na furaha na pia kuifanya amani kutawala kati yetu. Hivyo Mama Kanisa anapotupatia mwanzo mpya wa mwaka wa kiliturujia mioyo yetu isukumwe na maneno hayo ya Zaburi kwa kuanza upya na kuipyaisha tena safari yetu ya ukombozi. Mwanzo huu kama tulivyokazia hapo juu ni dokezo kwetu na kuendelea na juhudi za kudumu katika kupyaisha mahusiano yetu na Mungu na hivyo kudumu katika Yeye.

Katika ubatizo tunaungana na Kristo aliye upya huo wa uumbaji. Tumewekewa tayari mioyoni mwetu amana iliyotuingiza katika kuufurahia uwepo huo wa Mungu. Hii ina maana kwamba upya huo ambao nabii Isaya ameutabiri, upya ambao unatupatia furaha, unatupatia amani na kumleta Mungu mioyoni mwetu umekwisha kumiminwa ndani mwetu. Kwa neema ya Mungu tunafanyika upya katika Kristo. Mtume Paulo anatualika tugutuke na kuitambua hadhi hiyo: “saa ya kuamka usingizini imekwisha kuwadia”. Tunapouanza mwaka huu mpya wa kiliturujia tutambue kwamba safari ya ukombozi wetu ni dumifu, hakuna kulala hata kidogo na hivyo tuamke usingizini. Mwanzo huu mpya daima ututie shime ya kuyaangalia maovu ya ulimwengu huu, kugundua jinsi yanavyotuharibu, yanavyouharibu ulimwengu huu na yanavyotusambaratisha.

Mtakatifu Paulo Paulo anaendelea kusema kwamba: “usiku umeendelea sana, mchana umekaribia; basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru”. Tunapewa tena majira mapya ya kuistawisha nuru ya Kristo katikati ya giza linaloutawala ulimwengu huu. Paulo anasema kwa kujiamini kuwa mchana umekaribia ni kwa sababu anayo matumaini ya nguvu iliyopo ndani mwetu, yaani, mimi na wewe kwenda kuuangazia ulimwengu huu kwa nuru ya Kristo.

Hivyo si suala la kusikiliza tu maneno hayo na kuyafurahia utamu wake bali sasa sote tuinuke, tujivike silaha hizo za mwanga na kuanza kupambana na ulafi na ulevi wa mali, madaraka na sifa za ulimwengu huu, kupambana na uasherati na ufisadi ambavyo vinachafua aiba yetu ya kuitwa wana wa Mungu, ambavyo vinatugeuza kuwa watumwa wa miili na akili zetu, ambavyo vinauondoa upendo wetu kwa wenzetu, kupambana na ugomvi na wivu ambao hututenganisha na wengine huku tukijitukuza na kujiona tu bora zaidi yao.

Tuanze tena kwa nguvu na uchangamfu safari yetu. Tusiridhike na kile tulichokifanya na wala tusikatishwe tamaa na pale tulipolegea. Maneno ya mzaburi katika wimbo wa shangilio yawe ni nguvu kwetu tukisema “Ee Bwana utuoneshe rehema zako, utupe na wokovu wako”. Tuendelee na wajibu wetu wa kiinjili wa kupyaisha daima uhusiano wetu na Mungu na kutuunganisha sote kwake kusudi amani, uelewano, na upendo wa kweli vidumu nasi daima.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni Mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.