2016-11-25 14:02:00

Caritas Barani Ulaya ina matumaini juu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Barani Ulaya, Caritas Europa, linaguswa na changamoto zilizoko mbele katika kutafsiri na kutendea kazi mipango na malengo ya Agenda ya Umoja wa Mataifa kufikia mwaka 2030, Agenda inayohusu maendeleo endelevu. Kuguswa na kujali huku kunatokana na kutazama tofauti ya baadhi ya sera za Ulaya katika kukabiliana na changamoto mbali mbali.

Umaskini, njaa na athari za mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na kutozingatiwa kwa usawa na haki ni kati ya mambo yanayohitaji suluhu ya haraka ili kufikia malengo endelevu ya mwaka 2030. Kwa mantiki hiyo, Ulaya lazima iweke sera kereketwa kuanzia ngazi ya familia, kitaifa na mahusiano kimataifa, kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika mipango, mikakati na utendaji. Yamewasilishwa mapendekezo kwa ajili ya kupitishwa na kikao cha Umoja wa Ulaya kwa mwakani, 2017, katika kukabiliana na  changamoto za maendeleo. Lengo ni makubaliano ya Uragibishaji unaofumbata mahusiano ya umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Caribia na Pacifiki kuelekea malengo ya Ulaya ya mwaka 2020.

Caritas Ulaya inasema, ili kukabiliana na changamoto za wahamiaji na wakimbizi, sera za Ulaya lazima zizingatie mbinu na mikakati ya kupunguza umaskini, kuondoa kinzani, kulinda wahamiaji, kutoa elimu na fursa za kazi, kuwapokea wahamiaji na wakimbizi, kuwatunza na kuwafanya wawe sehemu ya jamii wanamojikuta. Maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2030, yatafikiwa kadiri ya matarajio kwa kujikita katika kujali na kuwanyanyua wanyonge, kuweka nguvu kwa maskini na walio katika mazingira hatarishi zaidi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.