2016-11-24 09:18:00

Salam, matashi mema na pongezi kwa Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia


Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima, hapo tarehe 20 Novemba 2016 ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili, amemtumia salam na zawadi ya masalia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, yaliyowasilishwa kwa niaba yake na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anasema, masalia haya ni msimamizi na mlinzi wake wa mbinguni, Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Papa anaendelea kumshukuru Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima kwa ushirikiano unaopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika maisha ya kawaida. Kimsingi majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthidox la Russia na Kanisa Katoliki yanaendeshwa na Tume ya pamoja ya Makanisa haya mawili na kwa mara ya mwisho mkutano wa tume hii umefanyika huko Chiet, Italia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anamtakia heri na baraka Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia na kumshukuru Mungu kwa kumpatia zawadi ya maisha na utume wa shughuli za kichungaji kwa Kanisa la Russia.

Baba Mtakatifu anampongeza kwa juhudi binfasi anazoendelea kuzishuhudia katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kama ule mkutano wao wa kwanza wa kihistoria uliofanyika mjini Havana, Cuba. Watakatifu Francisko wa Assisi na Serafino wa Sarov waendelee kuwasindikiza na kuwaombea. Mwishoni anamtakia matashi mema na amani katika maisha na utume wake. Kardinali Kurt Koch, akiwa ameambatana na Askofu mkuu Celestino Migliore, Balozi wa Vatican nchini Russia wamepokelewa mjini Moscow na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox.

Katika mazungumzo na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Russia, Patriaki Cyrrill amekumbuka kwa namna ya pekee, mkutano wake na Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba, ulioonesha kwa namna ya pekee, umoja na udugu; wasi wasi na mashaka yao juu ya hatima ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, Afrika ya Kaskazini na kwingineko ambako dhuluma, nyanyaso na vita yamekuwa ni matukio ya kila siku na kwamba, hii si tena habari inayopewa kipaumbele cha pekee na vyombo vya habari. Anasikitika kuona jinsi watu wanaovyoendelea kuteseka huko Siria na Iraq kutokana na vita ambayo imeendelea kwa muda mrefu sasa.

Ni matumaini ya Patriaki Cyrill kwamba, ushirikiano na malengo ya pamoja yanaweza kusaidia kupambana na vitendo vya kigaidi na hatimaye, amani kuweza kupatikana. Makanisa haya mawili yataendelea kushirikiana kwa karibu zaidi ili kupembua kwa kina na mapana madhara yaliyosababishwa na vita pamoja na machafuko ya kisiasa kiasi cha kuharibu makumbusho na nyumba za Ibada huko nchini Siria. Ni matumaini ya Kanisa la Russsia kwamba, Vatican kwa njia ya ushawishi wake kidiplomasia itawesa kusaidia kusitisha vita huko Mashariki ya Kati na hivyo kuwawezesha wananchi kurejea tena katika maisha yao ya kawaida anasema Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima katika mazungumzo yake na ujumbe wa Vatican nchini Russia uliomtembelea ili kuwasilisha zawadi na salam za matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapomshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 70 tangu alipozaliwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.