2016-11-24 14:51:00

Roho Mtakatifu chemchemi ya matumaini ya Kanisa!


Katika Mwaka wa Liturujia, Kanisa linaadhimisha Fumbo lote la Kristo Yesu, tangu Umwilisho hadi kurudi kwake kwa utukufu ili kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kipindi cha Majilio ni nafasi kwa waamini kulitafakari Fumbo la Umwilisho, Yesu alipozaliwa kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya mwanadamu. Hiki ni kipindi cha subira, imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Majilio ni kipindi kinachomwandaa mwamini kuadhimisha vyema Fumbo la Umwilisho, kwa toba na wongofu wa ndani, kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa njia ya tafakari ya kina ya Neno la Mungu!

“Roho Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini” ndiyo kauli mbiu itakayoongoza tafakari za kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2016 zitakazotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa nyumba ya Kipapa, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko kila Ijumaa, yaani: kuanzia tarehe 2 Desemba, 9 Desemba, 16 Desemba na tarehe 23 Desemba 2016. Tafakari hizi zitakuwa zinatolewa kwenye Kikanisa cha “Mama wa mkombozi” “Redemptoris Mater” kilichoko mjini Vatican.

Padre Cantalamessa anasema, hiki ni kipindi cha kujikatia kiu kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa kushibishwa na uzuri wake. Lengo ni kuendeleza tafakari kuhusu Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Roho Mtakatifu, ili Roho Mtakatifu aweze kupewa nafasi na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikaza kusema, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa. Viongozi mbali mbali wa Kanisa na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanaalikwa kushiriki kwa namna ya pekee katika tafakari hizi zitakazokuwa zinatolewa na Padre Raniero Cantalamessa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.