2016-11-24 15:53:00

Jihadharini na utamaduni wa uchu wa mali, rushwa na ufisadi!


Wakati waamini wanaadhimisha juma la mwisho la Liturujia ya mwaka wa Kanisa kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa Liturujia ya Kanisa kwa kipindi cha majilio, Mama Kanisa ametenga tafakari ya Neno la Mungu kwa siku za mwisho. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Mt. Martha mjini Vatican, siku ya Alhamisi, tarehe 24 Novemba 2016, amewaalika waamini kujihadhari na miungu ya rushwa, ufisadi, dhuluma, na tamaa ya fedha, ambavyo kavifananisha na mnyama wa vichwa saba anayetajwa kwenye masimulizi ya siku za mwisho, katika ufunuo wa Yohane (Rej., Ufunuo 13).

Utamaduni huo wa rushwa, ufisadi, dhuluma, na tamaa ya fedha ni ufalme ambao utaanguka tu, na anguko lake litakuwa kubwa. Utamaduni huo utakapoanguka pamoja na nguvu za shetani, aliye baba wa ufisadi, uonevu na tamaa, Mama Kanisa na watoto waaminifu wa Kanisa watashangilia kwa sauti juu ya anguko hilo, na kuimba wimbo wa wokovu: utukufu na nguvu vina Mungu, Bwana wa majeshi. Ibada kwa Mungu wa kweli itashinda na kudumu, ibada ya kweli ya waamini walio dhaifu, lakini ambao hawaharibiwa na dhambi, kwani wameambatana na Mungu wao wa kweli, anayewatia nguvu, anayewasamehe, anayewaongoza katika kweli, na kuwafanya washinde mbinu na hila za shetani. Ingawa ni wadhambi, wanatubu na kuomba msamaha, wanafanya juhudi za kuepuka mazingira ya dhambi, ili waupate wokovu ndani ya Kristu Yesu.

Baba Mtakatifu amesisitiza kujifunza sala ya kuabudu, kumuabudu Mungu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Ni sala yenye nguvu na ibada ya kweli inayomweka mwanadamu kimya mbele ya Mungu wake, na kumfanya kutambua yupo mbele ya muumba wake, naye mwanadamu ni kiumbe na mwana dhaifu, ambaye Mungu anampenda na anahitaji ushirikiano wa binadamu huyo ili kumkomboa.

Sauti ya tatu ya ushindi, ni ya malaika inayosema: heri walioalikwa kwenye karamu ya mwana kondoo. Sauti hii ni tulivu kama sauti ya mungu iliyozungumza na nabii Eliya katika mlima Horebu (Rej., IWafalme 19: 11-13). Sauti hii tulivu ya Mungu, ni sauti inayozungumza katika dhamiri ya mwanadamu katika ukimya wa kuabudu. Kadiri Injili inavyosimulia: yatakapoanza kutokea mambo haya, inueni vichwa vyeni juu kwani ukombozi wenu umekaribia (Rej., Luka 21, 28). Kwa maneno hayo Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kudumu katika uaminifu na kukaa tayari muda wote kumpokea Bwana, wakiwa wameinua macho juu kuupokea wokovu unaokaribia.

Na Padre Clestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.