2016-11-23 09:20:00

Viongozi wa kidini Afrika ya Kati wanapania kuendeleza amani!


Kardinali Dieudonné Nzapalainga, Askofu mkuu wa Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Imam Kobine Layama, na Mchungaji wa Protestanti Philippe Sing-Na, wanaharakati wa uwanja wa mahusiano na mazungumzano kati ya dini na imani mbali mbali nchini Afrika ya kati, siku ya Jumatatu tarehe 21 Novemba 2016, wamekutana katika Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Jijini Roma, mahali ambapo katika miaka ya hivi karibuni kumefanyika mazungumzano ya kutafuta suluhu ya kinzani za kisiasa na kijeshi kwa nchi ya Afrika ya Kati.

Siku ya Jumanne tarehe 22 Novemba 2016, nyakati za adhuhuri, wametembelea Msikiti wa Roma, uliopo Monte Antenne, ikiwa ni ishara ya mazungumzano na amani. Bwana Mauro Garofalo, mkurugenzi wa mahusiano ya nje katika Jumuiya ya Mt. Egidio amethibitisha kwamba, juhudi za Jumuiya hiyo katika kutafuta mazungumzano, amani, na kutoa misaada ya mahitaji msingi ya watu zitaendelea katika harakati za kuchangia maendeleo ya watu wa Afrika ya kati. Amani nchini Afrika ya kati bado ni changa, lakini watu wa nchi hiyo bado wana nguvu, moyo na ari ya ujana, hivyo elimu endelevu juu ya amani ni ya muhimu sana kwa nchi hiyo.

Imam Kobine Layama, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Afrika ya kati, kaitambua safari ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoifanya Novemba mwaka jana 2015 Bangui, kuwa ni tukio la kihistoria lililobadili historia ya nchi hiyo. Zaidi sana, heshima ya ukardinali aliyopewa Askofu mkuu wa Bangui, ni ishara ya hadhi na heshima ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaipatia nchi yao. Imam Layama anasema kwamba, kadiri ya Koran, maisha ni zawadi takatifu anayopewa mwanadamu, ndiyo sababu amekuwa mstari wa mbele kulinda maisha ya pamoja na ya amani kati ya Jumuiya za dini na imani mbali mbali.

Kwa mtazamo wa Mchungaji Philippe Sing-Na, hatambui chanzo hasa cha machafuko ndani ya nchi yao, lakini anao uhakika kwamba chanzo sio kinzani za kidini, kwani hapajawahi kuwepo kwa mitafaruku kati ya Wakristo na Waislam nchini humo. Mahusiano na mazungumzano kati ya dini hizo mbili, yamewafanya watu wa Afrika ya kati kuwa karibu zaidi na kujitambua kuwa ni ndugu wamoja na kwamba, tofauti zao za kiimani na kidini ni utajiri mkubwa na chachu ya maendeleo endelevu kiroho na kimwili!

Kardinali Nzapalainga ameishukuru Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa juhudi zake katika harakati za kutafuta mapatano nchini Afrika ya Kati, na kudhihirisha nguvu ya amani iliyo ndani ya viongozi wa dini. Iwapo watu watajikita katika kutazama vitu vinavyowatofautisha na kuwagawanya, hawatafika mbali. Mazungumzano, sala na mahusiano mazuri kati ya watu wa imani mbali mbali, ndiyo silaha ya kuteketeza machafuko na kufanya amani itawale, amesisitiza Kardinali Nzapalainga. Ujumbe wa kiekumene pamoja na waislamu waliofika Roma kwa ajili ya tukio la Askofu mkuu Dieudonné Nzapalainga kupewa heshima ya ukardinali, ni ishara kubwa ya udugu, upendo, mshikamano, mazungumzano, mahusiano na nia ya ujengaji wa amani na utafutaji maendelo kwa pamoja. Ishara ambayo inaangaza mbali zaidi ya Afrika ya kati, ishara ambayo ni mfano wa mazungumzano na udugu ambao lazima kuusisitiza kwa kila jamii.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.