2016-11-23 07:05:00

Mwongozo wa Ibada za Wakarismatiki Wakatoliki Uganda


Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga katika maadhimisho ya Alhamisi kuu kwa mwaka 2016, Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kuwa ni kumbu kumbu endelevu ya uwepo wake kati ya wafuasi wake, Daraja Takatifu la Upadre kwa jili ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa; utumishi unaomwilishwa katika huduma ya upendo, kielelezo kinachofumbata kwa dhati kabisa maisha na utume wa Yesu hapa duniani.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Askofu mkuu Lwanga alikumbusha kwamba,  kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa Katoliki, mafuta matakatifu yanatumiwa tu na Wakleri katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na wala si vinginevyo! Hii ilikuwa ni nafasi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda kutoa mwongozo kwa ajili ya wanachama  wa Karismatiki Katoliki, ambao wamekuwa wakilalamikiwa na familia ya Mungu nchini Uganda kwa kukiuka sheria, kanuni ma Mapokeo ya Kanisa.

Kuanzia sasa, wanachama wa Karismatiki Katoliki Uganda watakuwa wanasali katika maeneo maalum yaliyotengwa na kuainishwa na Maaskofu mahalia ili kuondokana na kashfa zinazoweza kujitokeza kutokana na Ibada zinazoadhimishwa na wanachama hawa. Ibada hizi zinapaswa kuongozwa na kusimamiwa na Wakleri, yaani: Maaskofu, Mapadre na Mashemasi na wala si vinginevyo. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya wanachama wanadai kwamba, wamepata “Upako” wa Roho Mtakatifu kumbe wanaweza kuongoza Ibada.

Maaskofu Katoliki Uganda wanawataka wanachama Wakatoliki wa Karisimatiki kuwa na utulivu wakati wa sala pamoja na kuacha mtindo wa kupiga makelele na kujigalagaza chini wakati wa maombi na ibada. Ibada ya kupunga pepo itafanywa tu watu waliopewa ruhusa na Maaskofu mahalia. Kwa wahubiri wanaotaka kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, wanashauriwa kupata kibali kutoka kwa Maaskofu mahalia kwani hawa ndio waliopewa dhamana na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaongoza, wanafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika maeneo yao.

Kumbe, Maaskofu mahalia wanao wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba, mafundisho yanayotolewa kwa niaba ya Kanisa Katoliki yanazingatia: Maandiko Matakatifu, Mapokeo, Sheria na Taratibu za Kanisa. Viongozi wa Wakatoliki Wakarisimatiki wanapaswa kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Maparoko wao, ili kuweza kupata taarifa za mara kwa mara za mikutano na sala za chama hiki cha kitume. Maaskofu wanakumbusha kwamba, umoja na Kanisa ni jambo muhimu sana kwa vyama vya kitume ambavyo ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo na kwamba haya ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Jimbo kuu la Kampala Uganda limewateuwa Monsinyo Expedito Magembe, Padre Athanasius Musajjakawa, Padre Lawrence Mubiru pamoja na Padre Dominic Mwebe kuwa ni Mapadre ambao wamepewa ruhusa rasmi ya kupunga mapepo Jimbo kuu la Kampala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.