2016-11-23 15:57:00

Mashirika ya kitawa na masuala ya kiuchumi!


Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuanzia tarehe 25- 27 Novemba, 2016 linaadhimisha  Kongamano la pili la Kimataifa kuhusu uchumi litakalofanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko mjini Roma kwa kuwakusanya wachumi wa Mashirika kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Kwa kuwa waaminifu kwa karama ya Shirika, mwelekeo mpya wa uchumi kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume”.

Huu ni mwendelezo wa kongamano la kwanza lililofanyika kunako mwaka 2014, kwa kutoa mwongozo wa kusimamia mali ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Hapa mkazo ulikuwa ni majiundo makini na endelevu kuhusu masuala ya kiuchumi mintarafu karama ya Shirika, ili kupyaisha mwelekeo wa sera na mikakati ya kiuchumi kwa kuzingatia pia ushuhuda wa kinabii! Hizi zitakuwa ni siku tatu za tafakari, majadiliano na upembuzi yakinifu kwa kutambua kwamba, miundo mbinu na rasilimali za Mashirika ya kitawa kama anavyosema Baba Mtakatifu zinatumika kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.