2016-11-22 14:33:00

Tema za maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani 2017- 2019


Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limetoa tema zitakazoongoza maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2019 zinazofumbata kwa namna ya pekee utenzi wa Bikira Maria, yaani “Magnificat”. Katika maadhimisho ya Siku ya 32 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017, Kanisa linatafakari kuhusu “Mwenye nguvu anenitendea makuu na jina lake ni takatifu” Lk. 1:19. Tema ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2018 ni “Usiogope, Mariam, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30. Na Mwaka 2019 ambapo maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatafanyika nchini Panama, yataongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” Lk. 1:38.

Hizi ndizo mada ambazo zimechaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika kipindi cha miaka mitatu, yaani kuanzia Mwaka 2017 hadi mwaka 2019. Huu ni mwendelezo wa tema ambazo zimefanyiwa kazi katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2016 kwa kujikita katika Heri za Mlimani. Katika hotuba yake kwa wafanyakazi wa kujitolea wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Cracovia,nchini Poland, 2015 Baba Mtakatifu alimtaja Bikira Maria ambaye vizazi vyote vinamwita Mwenyeheri kuwa ni mfano bora wa kuigwa.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na kumbu kumbu hai ya historia yao ya zamani, kuwa na ujasiri kwa mambo ya sasa na kuwa ni vyombo vya matumaini kwa siku za usoni. Tema hizi zinatoa kwa muhtasari safari ya maisha ya kiroho inayopaswa kutekelezwa na vijana wa kizazi kipya kwa kuangalia yaliyopita , 2017; yaliyopo, 2018 yajayo 2019, huku wakijitahidi kuambata fadhila za kimungu: imani, mapendo na matumaini. Tafakari hizi zinakwenda sanjari na mwelekeo wa Kanisa kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu itakayojikita kwa namna ya pekee katika masuala ya: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.