2016-11-22 09:18:00

Kanuni za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa Mwaka 2030


Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha mwaka mmoja tangu makubaliano ya Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa mwaka 2030, tarehe 5 Oktoba 2016, iliwekwa katika tovuti ya Umoja wa Mataifa, barua ya Vatican kuhusu malengo hayo ya maendelo endelevu kufikia mwaka 2030. Barua hiyo iliyotiwa saini na Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, imenuia kuchanganua baadhi ya kanuni za malengo ya maendeleo endelevu, ili kutathmini, kutafsiri na uwezekano wa kuzitendea kazi katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Kanuni ambazo barua hiyo imezidadavua ni pamoja na uelewa wa maendeleo fumbata ya mwanadamu, kuwatambua maskini kama wadau stahiki wa hatima yao wenyewe, kutoa nyenzo za kiroho na malighafi, kuheshimu kanuni ya haki, kulinda haki elimu katika mwanga wa hatima ya kiwango cha juu cha mwanadamu, kuheshimu utawala wa sheria, kutafuta suluhu za amani katika migogoro, kuhudumia wengine na kuheshimu mafao ya wengi, na kujenga msingi wa udugu wa familia kubwa ya wanadamu wote.

Hizi ni kanuni ambazo Baba Mtakatifu Francisko alizisisitiza kwenye hotuba yake kwa Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, mnamo tarehe 25 Septemba 2015, huku akiweka wazi kwamba, Agenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ni ishara muhimu ya matumaini, matumaini yatakayofikiwa, iwapo Agenda hiyo itafanyiwa kazi kwa uthabiti, katika ukweli na haki, na sio kuishia kwenye matamko tu bila kuyatekeleza.

Vatican inakubaliana na asilimia kubwa ya malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030, hata hivyo imependa kufafanua baadhi ya dhana zilizotumika katika Agenda hiyo, na kuweka wazi msimamo wake kwenye baadhi ya mambo. Katika kushughulikia malengo ya Agenda ya mwaka 2030, mwanadamu anapaswa kuwa ndiye kiini cha yote, dhana ya utu wa mwanadamu ikipewa kipaumbele, kutetea na kulinda wanaume, wanawake, vijana, mabinti, afya, haki na wajibu wa familia na wazazi na maendeleo fumbata ya mwanadamu.

Haki ya uhai na haki ya kuishi iliyo asili ya mwanadamu mwenyewe, inaingia mashakani na hatarini pale ambapo baadhi ya watu ndani ya jamii hawatambui uwepo wa uweza wa juu zaidi, bali wanajijali wao wenyewe. Ubinafsi unawafanya vipofu wa kushindwa kuona uhalisia wa ulimwengu. Ni lazima kuzingatia sheria ya maadili iliyo katika dhamiri ya mwanadamu, kuheshimu ukweli na hulka ya mwanamume na mwanamke. Ni dhahiri kwamba, haki za mwanadamu zinatokana na ukweli huo, na sio tamaa au vivutio binafsi vya kupendelea jinsia au mtindo fulani wa maisha.

Maendeleo ya mwanadamu hayalazimishwi, bali yanapewa nafasi ya kujifungua na kukua, huku kila mmoja akishirikishwa kwenye kila hatua. Kila mtu anazo karama na vipaji mbali mbali, anao uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya jamii, na ni lazima apewe fursa ya kuweka mchango wake. Kwa sababu hiyo, maskini ni lazima wawe sehemu ya msingi katika kushiriki maendeleo yao wenyewe. Ikumbukwe pia kwamba, maendeleo ni matunda ya mahusiano mazuri kati ya watu, kati ya makundi, kati ya wadau, na kati ya jamii mbali mbali. Haki siyo tu kumpa mtu ujira wake hasa kwenye mambo haramu kama biashara ya viungo vya mwanadamu au wanadamu wenyewe, ukahaba, dhuluma za ngono kwa watoto, madawa ya kulevya, biashara ya silaha, ugaidi, na uhaini mwingine wa kimataifa. Haki ni kumpa kila mtu kilicho chake, kwa kuzingatia utu wake, maadili ya jamii, uhuru wa dini na elimu, kuthamini tunu za ndoa na familia, lishe na afya bora.

Vatican inafafanua kwamba, iwapo kweli lengo ni kufikia maendeleo endelevu ya Agenda ya mwaka 2030, lazima kuepuka migogoro kwa kuheshimu utawala wa sheria. Suluhu za amani zitafutwe kwa kujali mazungumzano, midahalo, majadiliano, upatanisho, kuzuia matumizi ya silaha, kuzingatia uwazi kwenye biashara ili kuhakiki uhalali wake, na kuzuia kabisa biashara za silaha kwenye nchi zenye migogoro. Inahitajika hekima na busara katika kutambua kwamba mafanikio ya mwanadamu yanafumbatwa na huduma kwa wengine, huduma isiyo na chembe za ubinafsi, itiliwe mkazo heshima kwa viumbe vyote na kulenga mafao ya wengi. Heshima hii ikuzwe siku hadi siku kwa kujenga msingi mzuri wa udugu kati ya watu, kwa uelewa mzuri wa dunia kuwa ni Nyumba ya wote.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.