2016-11-21 14:59:00

Ushirikiano wa kimataifa ulenge kumkomboa mvuvi!


Fani ya uvuvi ni ya msingi sana katika kuhakiki usalama na kuchangia lishe bora kwa wanadamu na kukuza uchumi, ni ya muhimu kwa namna ya pekee kwa ajili ya kudumu kwa jumuiya za wavuvi wadogo wadogo kwenye mataifa mengi. Uvuvi ni kati ya biashara kubwa duniani leo, na umekuwa msaada kwa jamii nyingi sana. Utambuzi na uthamini huo wa uvuvi umesisitizwa na Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican, alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Siku ya Uvuvi Duniani, maadhimisho yaliyofanyika rasmi kwenye ofisi za Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, siku ya Jumatatu tarehe 21 Novemba 2016.

Mtazamo wa uchumi usisahau kulinda mtazamo mpana wa hali bora ya mwanadamu, inayokumbatiwa pia na utunzaji mzuri wa mazingira. Hivyo uvuvi salama wa kuzingatia taratibu na utunzaji wa maji safi, ni wajibu wa vyombo vyote vya ndani kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yeke ya kitume, Laudato sì, yaani "Sifa kwako" juu ya Utunzaji wa Nyumba ya wote, anasema: Bahari zinachukua sehemu kubwa ya maji ya sayari dunia, na ndani yake kuna viumbe hai kemkem ambavyo vingi bado havijafahamika vizuri kwa mwanadamu. Hata hivyo maji na viumbe hai hivyo vimo hatarini sababu ya uchafuzi wa mazingira na uharibifu usiojali unaofanywa na baaadhi ya watu (Laudato sì, n. 40).

Kardinali Pietro Parolin amesisitiza kuzingatia uvuvi unaojali mazingira, sababu ni muhimu kwa ajili ya afya njema, maendeleo ya kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Kuna upande wa haki na utu wa mwanadamu ambavyo vinakosewa heshima na kukanyagwa na baadhi ya mabepari katika fani ya uvuvi. Kuna wengi wanafanyishwa kazi kama watumwa, kwenye mazingira hatarishi na kulipwa mishara midogo. Wengi wa wafanyakazi hao ni wahamiaji na wakimbizi. Kardinali Parolini, anawaalika wafanyabiashara ya uvuvi kutotumia unyonge wa watu na kuwanyima haki zao, au kutoheshimu utu wao. Wafanyakazi wote watende kazi kwenye mazingira yanayofaa na kwa mikataba halali kisheria.

Vatican inaendeleza harakati zake za kutambua sehemu ambapo wafanyakazi katika fani ya uvuvi wananyanyaswa, ili kuinua sauti kwa niaba yao na kutetea haki zao. Vatican inawaalika viongozi wa kimataifa kuzingatia hali na haki za watu hao, ikiwa ni pamoja na kutoa vibali sahihi na kwa muda ili wahusika waweze kuzingatiwa kihalali na kwa haki zote. Sera za mataifa zizingatie utaratibu mzuri wa kujali wahamiaji na wakimbizi, uwezekano wa kuishi vizuri nchini humo, au kurudi kwa utulivu na kwa heshima nchini mwao ambapo hali inakuwa shwari.

Kila mmoja anaalikwa kushiriki na kuweka mchango wake kadiri ya uwezo na nafasi ili kutafuta haki, kudumisha mshikamano, kuthamini utu, na kuheshimu haki za kila mtu. Mshikamano na ushirikiano huo ulenge katika kumkomboa mvuvi kutoka hali ya utumwa na manyanyaso. Mataifa na watawala waheshimu makubaliano ya kimataifa na kuendeleza vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Lengo la mwisho ni kuhakikisha utataribu wa sheria unaheshimiwa hata baharini na ziwani, na shughuli zote zinazofanyika maeneo hayo. Kardinali Parolini kamalizia kwa kuwahakikishia FAO kwamba, Vatican ipo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha sehemu zote kwa kutumia vyombo vyake mbali mbali, ili wafanyakazi wa biashara ya uvuvi wapate uhuru na haki zao.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.