2016-11-20 10:24:00

Utenzi wa shukrani kwa maadhimisho ya Mwaka wa huruma!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, Jumapili tarehe 20 Novemba 2016, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa niabaya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa neema na baraka alizowakirimia. Amemshukuru Rais Sergio Mattarella kwa kuwakilisha ujumbe wa Italia pamoja na wageni waalika waliohudhuria katika Ibada ya kufunga maadhimisho haya. Amewashukuru viongozi wa Serikali na taasisi mbali mbali kwa ushirikiano wao wa dhati iliofanikisha maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewashukuru wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama; wahudumu katika mchakato wa mapokezi, wanahabari, wahudumu wa afya na watu wa kujitolea kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Amelishukuru Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya pamoja na wale wote walioshiriki kikamilifu kufanikisha maadhimisho haya. Baba Mtakatifu anawakumbuka hata wale waliochangia kwa njia ya sala ili kufanikisha maadhimisho haya! Hawa ni wagonjwa na wazee ambao wamesali daima na kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya ufanisi huu. Baba  Mtakatifu amewakumbuka Wamonaki wa ndani wanaposherehekea Siku yao, Jumatatu, tarehe 21 Novemba 2016. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na jicho la pekee kwa watawa hawa wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa njia ya sala, ili waweze kuwaonjesha mshikamano wa upendo: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mtumishi wa Mungu Padre Maria Eugenio wa Mtoto Yesu aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri huko Avignone, Ufaransa, Jumamosi, tarehe 19 Novemba 2016. Ni muasisi wa Shirika la Wakarmeli “watembea tupu” na taasisi ya “Bikira Maria Mama wa maisha”. Alikuwa kweli ni mtu wa Mungu, shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu iliyomwilishwa katika matendo ya huruma kwa jirani. Mfano, sala na maombezi yake viwasindikize waamini katika safari yao ya kiimani. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru waamini na watu wote waliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.