2016-11-20 11:31:00

Mnatumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Kristo kwa watu!


Jioni ya tarehe 18 mwezi Novemba mwaka 2016 wakati Jumuiya ya Wamisionari wa Shirika la Mapendo la Warosmini wakiadhimisha kumbukumbu ya Mwenyeheri Antonio Rosmini mwanzilishi wa Shirika hilo, maisha katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Porta Latina mjini Roma, yalianza kupata sura mpya wakati Mama Kanisa alipoongeza watenda kazi katika shamba lake kwa kupata Mashemasi wawili wapya. Hawa ni Shemasi Wilhad Casmir Shayo na Nicas Francis Shirima wa Shirika hilo la Warosmini katika mikono ya  Askofu mkuu Antonio Giuseppe Caiazzo wa Jimbo kuu  la Matera-Irsina, nchini Italia ambaye pia ni mwanashirika wa Shirika la Mapendo.

Katika mahubiri yake Mhashamu Caiazzo aliwasisitizia neno moja kuu la kuwa waenezaji wa furaha ya Kristo kwa watu wote. Mhashamu Askofu mkuu Caiazzo aliwahasa mashemasi hawa wapya kwamba furaha hiyo inapaswa kuanzia ndani mwao kwa kuupokea wito huu wa Kristo na kuukubali si kwa ajili ya vipawa vyao bali kwa sababu Bwana Yesu mwenyewe amabye anawaita ndiye atawawezesha kuifikisha hiyo furaha yake. Mhashamu Caizazzo alisema “Shemasi mwenye huzuni atawafanya wakristo kuwa na huzuni, Padre mwenye huzuni atawafanya waamini kuwa wenye huzuni na Askofu mwenye huzuni atawafanya waamini kuwa wenye huzuni” na hizo akawaasa wadarajiwa hawa kujazwa na furaha ya Kristo na kwenda kuieneza kwa watu wote.

Akitoa Neno la Shukrani kwa niaba ya mwenzake Shemasi Wilhad aliishukuru Jumuiya ya Kanisa kwa sala zao na kwa kuungana nao katika safari nzima hadi kuifikia siku hiyo ya kupokea daraja ya Ushemasi. Kwa pamoja wamemshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na utume katika Kanisa. Wote wamekiri kwamba, si kwa mastahili hayo bali ni neema za Mungu na kwa wanazidi kuomba maombezi ya waamini ili kusudi hizo neema za Mungu ziwamiminikie na kuuendelea kutunza wito wao. Wamezidi kuomba sala  ili kuifikia daraja takatifu ya Upadre hapo baadaye kwa kadiri ya mipango na taratibu za  Mama Kanisa.

Shemasi Wilhad Shayo amezaliwa mnamo tarehe 06 Agosti 1980 huko Moshi Mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania akiwa ni mtoto wa kwanza kati  ya watoto saba wa mzee Casmiri na Mama Yovitha. Alijiunga na Shirika la Mapendo la Warosmini mnamo terehe 15 Septemba 2003. Baada ya majiundo ndani ya Shirika hili aliweka nadhiri zake za mwanzo tarehe 17 Juni 2006 katika nyumba yao ya Novisiati huko Lushoto Tanga nchini Tanzania. Baadaye alitumwa kwa masomo ya shahada ya kwanza katika masomo ya Sayansi akibobea katika fani za fizikia na kemia na kisha kuwa mkufunzi katika shule ya Warosmini huko mkoani Tanga. Mnamo tarehe 12 Januari 2013 alifunga nadhiri za daima na baadaye tarehe 11 Septemba 2013 alitumwa mjini Roma nchini Italia kwa ajili ya kujifunza masomo ya Falsafa na Taali Mungu katika Chuo cha Mtakatifu Beda kilichopo mjini Roma.

Shemasi Nicas Francis Shirima amezaliwa mnao tarehe 04 Novemba 1983 katika Parokia ya Mrao Jimboni Moshi nchini Tanzania. Baada ya masomo yake ya awali katika shule ya Msingi Mombwe na Sekondari za Ibukoni na Old Moshi alijiunga na Shirika la Warosmini mnamo 15 Agosti 2006 katika malezi ya upostulanti huko Gare. Aliweka nadhiri za kwanza huko Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga mnamo tarehe 29 Juni 2009 siku ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Kisha akaelekeza nchini Kenya kwa masomo ya Falsafa yakiambatana na uzoefu wa kitume katika nyanja mbalimbali. Baadaye litumwa mjini Roma nchini Italia kwa masomo ya Taalimungu. Tarehe 18 Novemba 2015 alifunga nadhiri zake za daima katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Porta Latina Jimbo kuu la Roma.

Na: Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.