2016-11-19 11:33:00

Makardinali wapya: Kupenda, kutenda wema, kubariki na kusali ndo wajibu wenu


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya 17 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 19 Novemba 2016 kama awamu ya kwanza ya kufunga Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu amekazia umuhimu wa mafundisho ya Yesu Mlimani aliyetaka kugusa undani wa maisha ya mitume wake, ili hatimaye,  waweze kuugundua Uso wa huruma ya Mungu, ili nao wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kama alivyo Baba wa milele!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika mwaliko huu, Yesu amekazia mambo kadhaa ambayo Mitume wake wanapaswa kuyatekeleza kwa dhati kama mhimili wa huruma ya Mungu: kupenda, kutenda wema, kubariki na kusali. Haya ni mambo ambayo kama viongozi wa Kanisa wanayatekeleza na kuyamwilisha katika maisha na utume wao wa kila siku kama sehemu ya mazoea. Lakini Yesu anakaza kusema, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukia; wabarikini wale wanaowalaani na waombeeni wale wanaowaonea ninyi!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, ni rahisi sana kwa mtu anayekutana na adui au mpinzani wake, jambo la kwanza ni kutaka kumfuta akilini na moyoni mwa mwake! Lakini mambo ni kinyume kabisa katika mafundisho ya Yesu kuhusu adui, watu wanaowachukia na kuwalaani na wanaambiwa kwa namna ya pekee: kuwapenda, kuwatendea wema, kuwabariki na kuwaombea. Hiki ni kiini cha chemchemi ya furaha na nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Adui ni mtu anapaswa kupendwa kwani moyoni mwa Mwenyezi Mungu kuna watoto wake wapendwa na wala hakuna adui, kuta hizi za utengano zinajengwa na binadamu wenyewe.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo wa Mungu ni aminifu na unawakumbatia watu wake wote; anaendelea kuwapenda wema na wabaya; wenye haki na wanaokosewa haki zao msingi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu amewapenda upeo, kiasi cha kuwapatia utambulisho wa kuitwa wana wa Mungu, hata pale ambapo bado walikuwa ni adui zake, aliwaonesha upendo usiokuwa na kifani. Upendo huu usiokuwa na mipaka ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu kutokana na moyo wa binadamu unaotaka daima: kuhukumu, kugawanya au hata wakati mwingine kulaani! Mwenyezi Mungu anaendelea kuwapenda wote pasi na ubaguzi, chachu ya utume endelevu wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kusisitiza kwamba ulimwengu mamboleo unakabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali, lakini suluhu inayopewa kipaumbele cha kwanza ni kuwatenga watu. Kwa mfano; wahamiaji na wakimbizi wanaonekana kuwa ni adui na watu wanaohatarisha amani na usalama wa watu. Wanageuka kuwa ni adui kwa vile tu wanatoka nje ya nchi, wana rangi na lugha tofauti; hali yao ya kijami; ni adui kwa sababu wana mawazo na imani tofauti. Dhana hii ya uadui inawafanya watu kuishi, kutenda na kuwa ni sehemu ya mwenendo wa maisha. Lakini chanzo cha mambo yote haya ni dhana ya uadui na baadaye utofuti unageuka kuwa chuki, hatari na hatimaye, vita. Kutokana na dhana ya vita na uadui kuna watu wengi wanaoendelea kujeruhiwa, hususan miongoni mwa watu wasiokuwa na sauti; machozi yao yamekauka sawa na kilio cha samaki majini; hawana sauti tena inayosikika, wamebaki na kwikwi kinywani mwao kutokana na hali ya watu kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, chuki, uadui na uhasama vinaendelea kusababisha madhara makubwa kati ya watu; kati yao kama viongozi wa Kanisa na Jumuiya zao; Mapadre wao na hata katika mikutano yao. Kirusi hiki cha uadui kinaratibu namna ya kufikiri, kusikia na kutenda, changamoto ya kuwa makini kutokana na mambo haya, ili yasipate nafasi katika sakafu ya nyoyo zao, kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume kabisa cha amana, utajiri na Ukatoliki wa Kanisa wanaoweza kuugusa kwa mikono yao katika Baraza la Makardinali.

Baba Mtakatifu anasema, Makardinali ni watu wanaotoka nchi za mbali, wana tamaduni, rangi, mila, lugha, desturi na hali za kijami zinazotofautiana sana; wanafikiri na hata wakati mwingine wanaadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika kwa Ibada tofauti; lakini katika yote haya hakuna hata jambo moja linalowafanya kujisikia kuwa ni adui na matokeo yake, ni kuona utajiri mkubwa wa Kanisa. Yesu anaendelea kuteremka katika mabonde na anataka kujimwilisha katika maisha yao, ili waweze kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu. Yesu anaendelea kuwaita na kuwatuma kwa watu wao kama alama ya upatanisho.  

Kanisa linawahamasisha Makardinali kufungua macho yao ili kuangalia madonda ya ndugu na jirani zao waliopokwa utu na heshima yao. Mwishoni Baba Mtakatifu nawakumbusha Makardinali wapya kwamba, njia ya kwenda mbinguni inaanza katika maisha ya kila siku kwa kujisadaka bila ya kujibakiza; katika hali ya ukimya kwa kila ambacho wako. Kilele cha maisha yao ni ubora wa upendo na maisha ya watu wa Mungu, ili kuwageuza kuwa ni watu wenye uwezo wakusamahe na kujipatanisha; daima wakikumbuka kwamba wanaitwa kuwa na huruma kama Baba wao mbinguni alivyo na huruma.

Kama kuna jambo ambalo linastahili kuzisuta dhamiri zao ni ukweli kwamba, kuna watu wengi wanaishi bila ya kuwa na nguvu, mwanga na faraja inayobubujika kutokana na urafiki wao na Kristo Yesu; wala kuwa na Jumuiya ya imani inayowasaidia; bila maana na lengo katika maisha. Mara tu baada ya Ibada, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Makardinali wapya wakiwa wamepanda kwenye mabasi mawili, walikwenda moja kwa moja hadi kwenye Monasteri na Mater Ecclesiae ili kumsalimia Papa mstaafu Benedikto XVI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.