2016-11-18 07:07:00

Wayesuit wameamua kujifunga kibwebwe kuganga madonda ya walimwengu!


Tafakari ya Wajesuiti leo ni ile inayowaongoza kwenye kuitazama dunia kwa macho ya maskini na kushirikiana nao ili kukuza maisha ya kweli. Tafakari inayowaalika kwenda pembezoni mwa jamii na kutafuta namna ya kukabiliana na upamoja wa changamoto unaokuwa kikwazo kupatikana kwa hali ya kawaida ya maisha kwa wanadamu wengi, kiasi cha kuhatarisha maisha kwenye sayari dunia. Sehemu hiyo ya mahubiri anapotilia mkazo Padre Arthur Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika la Wajesuiti, anawaalika wanashirika hilo kupambana na nadharia na fikra finyu zisizo na mashiko katika dunia ya leo.

Misa Takatifu hiyo ya kufunga mkutano mkuu wa 36 wa Shirika la Wajesuiti, imeadimishwa Siku ya Jumamosi iliyopita, tarehe 12 Novemba 2016, katika Kanisa la Mtakatifu Inyasi, lililoko Jimbo kuu la Roma.

Padre Arthur Sosa Abascal kahimiza kwamba, utume wao kwa sasa hauwezi kukwepa matumizi ya fikra pana, kwani macho ya huruma wanayozawadiwa katika kufanana na Kristu msalabani, yatawasaidia kupambanua yale yote yanayopelekea mateso kwa wanaume na wanawake katika nyakati hizi za sasa. Kuna changamoto kubwa kuwa mtumishi wa Upatanisho katika dunia ambamo madonda ya vita yanaendelea kuchimbika, na mateso ya wakimbizi yanazidi kuumiza watu. Mbaya zaidi, siasa ambayo ni sanaa ya kuhangaikia mafao ya wengi badala ya manufaa binafsi, inaendelea kuwa dhaifu katika kusaidia wanadamu.

Ishara zinazaoendana na utangazaji Injili, ni zile za kufukuza mapepo ya udanganyifu yasiyoonesha uhalisia wa mambo. Ni muhimu kujifunza lugha mpya ili kuelewa maisha ya watu mbali mbali na kuwashirikisha habari njema ya wokovu, kasema Padre Arthur. Amehitimisha kwa kusema kwamba, wakiifungua mioyo yao katika utendaji wa Roho Mtakatifu, na akili zao kwa Ukweli wa Upendo wa Mungu, hawatakunywa sumu ya nadharia za uonevu, unyanyasaji kati ya watu, unyonyaji na uharibifu wa maliasili. Imani ndani ya Kristu aliyeteswa, kufa na kufufuka, itawatia nguvu ya kuchangia uponyaji wa dunia ya leo, wakishirikiana na wengi wenye nia hiyo njema.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.