2016-11-18 16:20:00

Watanzania: Imarisheni umoja, upendo na mshikamano!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka watalaamu wa ujenzi wa mradi wa nyumba za makazi Magomeni watumie utaalamu wao vizuri na wakamilishe kwa wakati. Ametoa agizo hilo  Ijumaa, Novemba 18, 2016 wakati alipokagua ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na wataalamu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amewataka wataalamu hao waendelee kufanya kazi hiyo kwa kufuata misingi ya weledi wa taalauma yao kwani Serikali inawaamini. “Muhimu mjue kwamba mmepewa dhamana hii kubwa ya kukamilisha ujenzi huu ili wananchi waliokuwa wanaishi hapa waweze kurudi katika makazi yao,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA, Mhandisi Edwin Nnunduma amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itahusisha majengo matano ya makazi. “Kati ya majengo haya matano, manne yatakuwa na ghorofa nane na moja litakuwa na ghorofa tisa, ambapo wakazi zaidi ya 600 waliokuwa wanaishi eneo hili tangu zamani watakabidhiwa,” amesema.

Mhandisi Nnunduma amesema majengo hayo yanajengwa kwa teknolojia ambayo imezingatia uwezo wa wakazi wake ambapo ina majiko yanayoweza kutumia kuni na mkaa. Amesema mradi huo ambao unajengwa kwa awamu tofauti utahusisha ujenzi wa nyumba za makazi, maduka makubwa na ya kisasa pamoja na ofisi. Mhandisi huyo amesema awamu ya kwanza iliyoanza Oktoba Mosi, mwaka huu inahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo ambayo inatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani.

Wakati huo huo Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka Waislamu nchini waendelee kushirikiana na Serikali kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini. Aidha, amewasihi waamini wa dini ya Kiislam kuimarisha umoja, upendo, mshikamano miongoni mwao kwa kushirikiana na jamii zinazowazunguka bila kujali tofauti zao za kiimani.  Ametoa wito huo Ijumaa, Novemba 18, 2016 wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Amesema uwepo wa dini umewezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu hivyo kila mmoja ahakikishe suala hilo linaendelezwa.  Pia amewashauri waumini na viongozi wa dini kuzingatia maadili ya dini ili kuepusha migongano isiyo ya lazima hasa taasisi zinapokuwa na miradi. Waziri Mkuu alitolea mfano msikiti huo wa Kichangani chini ya Sheikh Walid umeweza kusuluhisha hitilafu ya wenyewe kwa wenyewe bila kukimbilia Serikalini au mahakamani kusuluhishwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Waislamu wana jukumu la kuwafunza elimu ya dini watoto wao na kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema. Amesema dini inajenga maadili mema kwa mtoto na kumwezesha kukua katika misingi ya uvumilivu na inamuwezesha kumtambua Mwenyezi Mungu.  “Nimefarijika kuona vijana wengi wameshiriki katika sala hii ya Ijumaa. Nawaomba wazazi waendelee kuelimisha watoto umuhimu wa kufanya ibada,” amesema. “Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” amesema. Waziri Mkuu amewaomba waumini hao waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.