2016-11-18 07:39:00

Tubuni na kuiamini Injili ni mwaliko endelevu kwa waamini!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka kwa waamini kujitahidi kuishi huruma kama Baba wa mbinguni, ili kushiriki kikamilifu katika mpango wa upyaisho wa maisha ya kiroho unaodai kwanza kabisa juhudi ya toba na wongofu wa ndani; ili kuambata huruma, upendo, furaha, msamaha na amani ya ndani inayobubujika kutoka kwa Baba mwenye huruma kwa njia ya Kanisa lake ambalo kimsingi ni chombo na shuhuda wa huruma ya Baba!

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kimekuwa ni kipindi cha mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, kiini cha Injili ya Kristo. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Baba wa mbinguni ni ya milele na fumbo ambalo kimsingi mwamini anapaswa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yake ya kila siku. Huruma ya Mungu ni utenzi wa sifa kwa wenyeheri na watakatifu; watu wanaojitambua kwamba wanahitaji kuzamishwa katika bahari ya huruma ya Mungu, tayari kuambata na kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao.

Askofu Ngalalekumtwa anakaza kusema, huruma haswa ndilo jina na utambulisho wa Mwenyezi Mungu; huruma inayomaainisha pia msamaha kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; watu ambao wanaweza kutubu na kukimbilia huruma ya Mungu, ili nao waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao, kwa kuanza maisha mapya. Waamini waendelee kumwilisha huruma ya Baba katika maisha haya baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuiga mfano wa Baba mwenye huruma na mwana mpotevu aliyegundua kwamba, amekosa mbele ya Mungu, akaamua kuwa na msimamo mpya wa maisha, kwa kutubu na kumwongokea Mungu yaani “metanoia”

Askofu Ngalalekumtwa anaendelea kufafanua kwamba, kila mtu anahitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Waamini waendelee kutafakari mambo yanayokwamisha mahusiano yao na Mungu pamoja na jirani, ili katika ukweli na unyoofu wa moyo waweze kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu yadumu milele! Kila mara waamini wanapojikwaa, wakateleza na kuanguka dhambini, wawe na ujasiri wa kusimama tena na kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu, kinachoboreshwa kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, maisha adili na matakatifu yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Hiki ni kielelezo makini cha ima ni tendani anasema Askofu Ngalalekumtwa katika mahojiano maalum na Radio Vatican!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.