2016-11-18 14:17:00

Maadhimisho ya Sherehe za Kufunga Mwaka wa Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, tarehe 20 Novemba 2016 atafunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ibada inatarajiwa kuanza majira ya saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya. Tukio  hili la kihistoria linatanguliwa na Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni.

Ibada hii inaadhimishwa Jumamosi, tarehe 19 Novemba 2016 na itaanza majira ya saa 5:00 asubuhi kwa saa za Ulaya. Matukio yote haya yatatangazwa moja kwa moja kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican katika kiwango na ubora wa kuridhisha, ili familia ya Mungu iweze kushuhudia matukio haya anasema Monsinyo Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican. Kwa mara ya kwanza kituo cha Televisheni cha Vatican kwa kushirikiana na Radio Vatican kitaweza kurusha matangazo haya moja kwa moja kutoka Vatican.

Kundi hili la wataalam linashirikiana na wafanyakazi katika sekta ya mahusiano ya kimataifa kama sehemu ya utekelezaji wa azma ya Baba Mtakatifu Francisko anayependa kuona kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican vinashirikiana kwa karibu ili kutoa ubora na viwango vya kuridhisha.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei yanaelekea ukongoni, lakini bado waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaendelea kuhamasishwa na Mama Kanisa kujizamisha katika bahari ya huruma ya Mungu. Ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko anataka kuhakikisha kwamba, Kanisa linawekeza kikamilifu katika matumizi ya vyombo vya habari, ili huruma na upendo wa Mungu uweze kuwafikia na kuwaambata watu wengi zaidi, hasa wale ambao wanaishi pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.