2016-11-18 14:52:00

Kumbatieni ufukara wa Kikristo, fedha na mali iwe ni kwa ajili ya huduma!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 18 Novemba 2016, Ibada ambayo ilikuwa maalum kwa Makatibu wa Balozi za Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia, amewakumbusha kwamba Jamii kamwe haiwezi kuwasamehe Wakleri wanaomezwa na malimwengu kwa kutawaliwa sana na uchu wa mali na madaraka! Makatibu hawa wako mjini Roma, ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumapili ijayo, wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu.

Injili ya siku inamwonesha Yesu Kristo akiwafukuza watu mbali mbali ambao waliligeuza Hekalu kuwa kana kwamba ni pango la wevi na wanyang’ayi. Uchu wa mali na fedha ni mambo ambayo kimsingi yanapinga sana na Ufalme wa Mungu, kwani mtu hawezi kuwatumikia mabwana wawili yaani Mungu na fedha. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Hekalu ni nyumba ya Sala, nyumba ya huruma na mapendo ya Mungu, lakini kishawishi cha fedha na uchu wa mali, daima kinawaandama hata Wakleri katika maisha na utume wao, hali inayoweza kuhatarisha maisha na utume wa Kanisa kwa kuwaacha Wakleri wakiwa hawana furaha ya ndani wala ari na moyo wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu.

Kristo Yesu, njia, ukweli na uzima ndiye peke yake anayeweza kuwapatia furaha ya kweli katika maisha na utume wao kama Mapadre. Baba Mtakatifu anawaonya Wakleri kutokuwa na uchu wa fedha na mali, kwani kamwe waamini hawatawasamehe dhambi hii kubwa. Wanaweza kuwasamehe mapungufu mengine ya kibinadamu, lakini uchu wa fedha na mali, ni vigumu sana kupata msamaha. Inasikitisha kumwona Padre akiwa kitandani, “hoi bin taabuni”, lakini ndugu zake wanapambana kugawana mali yake.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri kufanya maamuzi ya ujasiri kuwa na fedha kiasi itakayowasaidia katika maisha na utume wao. Wajitahidi kuwa waaminifu, ili kweli fedha hii iwe ni matunda ya jasho lao linalotokana na uaminifu kwa Mungu na Kanisa, mwaliko wa kuambata ufukara wa Kikristo, ili fedha na mali iwe ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.